Mfungaji bora kule Biological, Joseph Atsere

Klabu ya Biological imewasha moto kwenye awamu ya pili ya MU Supa Ligi, kwa kudhalilisha na kuhujumu tatu bora za kundi la ‘Magharibi’. Vijana hao wanaopiga zoezi kule Pavilion, wamekuja na ari mpya hivi karibuni, ingawa walinyong’onyea hapo mwanzo. Chini ya ukufunzi wa Hillary, Biological wamezoa pointi tano katika mechi tatu walizocheza na Upper Hill, Wazee na Wasafi.


Tarehe mbili Novemba, Upper Hill nusura wapate kichapo kutoka kwa hao hao Biological, walipowapumzisha Edwin Maru, Gilbert Kipng’etich na kipa Alfred Ndemo. Kipute hicho kilichoandaliwa ugani Upper Hill A, kilishuhudia mwuaji Joseph Atsere akiwafunga Upper Hill mabao mawili kipindi cha kwanza, matokeo yaliyosalia hadi mapumziko. Hata hivyo, ujio wa Edwin Maru, Afred na “Kante” kipindi cha pili uliokoa jahazi la Wanaupper Hill lililokuwa linazama. Maru alifunga penalti muhimu iliyolazimisha sare ya mabao mawili.

Wanabiological ugani Pavilion, baada ya mazoezi


Hali kadhalika, Ijumaa ya wiki jana Wazee wa Kazi walilishwa pilipili walipocharazwa mabao mawili kwa nunge na vijana wa Hillary. Mastaa wa Wazee Moses Karani, Federico Muia ma wengineo waliambulia patupu, huku Atsere wa Biological akicheka na wavu. Nyota huyo anajivunia mabao saba hadi sasa na amekuwa nguzo muhimu katika mechi za Biological. Hata hivyo, mbinu zake za ufungaji zilizibwa na kipa Brian Asuka Jumapili, walipotoka sare tasa na Wasafi. Vile vile, ndoto ya Wasafi kuwapiku Upper Hill ilididimizwa kwa sare hiyo, Eugene, Patrick, Benson na “Yorke” wakishindwa kupata bao.


Katika matokeo ya Jumamosi, Boca Seniors waliandikisha sare ya bao moja na Wayia kule Pavilion, Redstars ikainyuka Angaza, Wasafi wakanyuka Wazee, nao Wakataji wakakandamiza Tyre powers. Jumapili, Wazee walirejea kwa hamu na kuwacharaza Upper Hill mawili kwa nunge, Boca Seniors wakanyorosha Tedians, nao Field Marshalls wakazidisha masaibu ya Tyre powers kwa ushindi wa mabao manne bila jibu.

Leave a Comment