BALE AMEKUWA NA MAJERAHA 19 TANGU KUJIUNGA NA REAL MADRID

Gareth Bale

Ni wazi kuwa maji yamezidi unga kwenye taaluma ya Gareth Bale, kwani majeraha yanazidi kumwandama na kumganda kama kupe.

Nyota huyo mzaliwa wa Wales, alijiunga na Real Madrid mwaka wa 2013 kutoka Tottenham, kwa kima cha Euro milioni mia moja (€100M).

Bale hajachezea Los Blancos tangu mwezi Septemba, alipoumia katika mechi ya kombe la klabu bingwa dhidi ya Borussia Dortmund. Hata hivyo, mshambulizi huyo alichezea Wales majuzi katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia, na alionekana dhabiti.

Bale alikaribishwa Santiago Bernabeu kwa mazoezi ya mechi ya wikendi dhidi ya Atletico ila aliumia tena Alhamisi.

Jeraha hilo ni la kumi na tisa tangu Bale kujiunga na Real Madrid na mengi ya majeraha hayo huwa ya shavu la mguu; manane ya kushoto na mawili mguu wa kulia. Vile vile, majeraha ya mgongo, kiuno na goti yamemkumba.

Makocha Carlo Ancelotti, Rafa Benitez na Zinedine Zidane wamekuwa na imani na Bale ila imemlazimu Zidane kutomwanzisha kwa hofu ya jeraha kutokea. Kwa sasa, uvumilivu na huruma ya Real Madrid kwa Bale umeanza kupungua na klabu hiyo iko radhi kumwuza.

Hebu tuangalie historia ya majeraha ya Gareth Bale:

2013- 2014

Majeraha : 6
Mechi alizocheza: 40. Alizokosa : 17
Mabao : 22. Aliyochangia : 12

Huu ndio msimu Bale alitua Madrid na hakuwa dhabiti kwani alikuwa hajacheza mno, kwa sababu uhamisho wake ulicheleweshwa. Bao lake la kwanza lilikuwa dhidi ya Villarreal, Septemba na shavu lake la mguu liliumia tena kabla ya kumenyana na Getafe.

Wiki chache baada ya kupona aliumia tena dhidi ya Atletico Madrid, jeraha lililomweka nje mwezi mzima.
Oktoba msimu huo, mtandao wa Marca ulitoa taarifa kuwa majeraha ya Bale yalisababishwa na kusimama kwa muda mrefu, jambo ambalo Real ilipuuza walipomsajili.

Hata hivyo, Bale alifunga bao la ushindi kwenye fainali ya Copa Del Rey dhidi ya Barcelona na kuipa Real taji. Kwa mara nyingine Bale aliipa Real Madrid Kombe la klabu bingwa la Decima, alipofunga bao la ushindi dakika za mazidadi.

2014- 2015
Majeraha: 2 Mechi alizocheza : 46 Alizokosa : 12
Mabao : 16. Aliyochangia: 10

Jeraha la kwanza msimu huu kwa Bale lilitokea mazoezini, alipoumia mgongoni baada ya kupiga fataki. Jeraha hilo lilimkosesha mechi nne, moja dhidi ya Liverpool kwenye klabu bingwa na dhidi ya Barcelona kwenye Clasico, mechi ambayo Real Madrid ilishinda mabao matatu kwa moja.

Ancelotti alifutwa mwishoni mwa msimu huu na mashabiki walimlaumu Bale baada ya kupoteza kwa Juventus kwenye nusu fainali ya klabu bingwa.

2015- 2016
Majeraha: 6 Mechi alizocheza: 29  Alizokosa : 22  Mabao : 19. Aliyochangia : 12

Kocha mpya, Rafa Benitez alianza kipindi chake kwa kusema kuwa Bale angekuwa nguzo kuu kwa kikosi chake, lakini nyota huyo aliumia tena kwenye shavu la mguu. Jeraha hilo lilimkalisha mkekani kwa Mechi nane kati ya Septemba na Oktoba.

Kwa bahati nzuri, Bale alipona na kuichezea nchi yake ya Wales dhidi ya Bosnia na Andorra, kwenye mechi za kufuzu Euro 2016.

Kwa mara nyingine, Bale aliumia kwenye goti, mgongo na shavu la mguu na kukaa nje mwezi Januari na Februari. Licha ya majeraha hayo, Bale alifunga bao la ushindi dhidi ya Barcelona, Camp Nou huku akifunga la kipekee dhidi ya Manchester City kwenye Kombe la klabu bingwa.

Bale atakumbukwa mno kwa kufunga penalti kwenye fainali ya klabu bingwa, Real ilipoilaza Atletico Madrid na kutawazwa ubingwa.

Bale na Cristiano Ronaldo katika mechi ya awali

2016- 2017
Majeraha: 3 Mechi alizocheza : 25 Alizokosa : 35
Mabao: 9. Aliyochangia: 3

Msimu huu Bale alianza katika hali nzuri huku akiongeza kandarasi ya miaka sita na miamba hao wa Uhispania. Alikuwa mshambulizi bora kwa Real wakati huo kwani mshambulizi mwenza, Ronaldo alikuwa ameanza msimu kwa unyonge.

Hata hivyo, hali hii haikudumu kwani aliumia tena kwenye kano la kifundo cha mguu, Real Madrid ilipomenyana na Sporting Lisbon.

Ingawa Real Madrid ilishinda taji la klabu bingwa, Bale hakuwa amechangia sana na Isco alionekana kuchukua nafasi yake kabisa.

2017- 2018
Majeraha: 2 Mechi alizocheza: 9. Alizokosa: 8
Mabao : 3. Aliyochangia: 3

Tangu msimu kung’oa nanga, Bale amekuwa shwari na alifunga bao stadi na kuchangia jingine dhidi ya Deportivo la Coruna kwenye Laliga. Kwa bahati mbaya, Bale aliumia wikendi iliyofuata dhidi ya Valencia, mechi iliyokwisha kwa sare ya mabao mawili.

Matumaini ya Zidane yalipata afueni Bale alipopona na kurejea dhidi ya Dortmund kwenye kinyang’anyiro cha klabu bingwa. Mshambulizi huyo alifunga bao kwenye mechi hiyo, lakini alianza kuchechemea mwishoni mwa mechi.

Nyota huyo alitajwa kuwa na jeraha kirasmi alipojiunga na kikosi cha Wales katika maandalizi ya mechi za kufuzu Kombe la Dunia.

Real Madrid imetumia zaidi ya Euro milioni moja kwa majeraha ya Bale na ni wazi kuwa wako tayari kumwuza ili kerejesha senti hizo. Klabu kadha ikiwemo Tottenham na Manchester United zimeonyesha nia ya kumsajili.

 

 

Leave a Comment