Mshambulizi wa timu ya taifa ya Harambee Stars na klabu ya Girona, Michael Olunga ameandikisha historia hii leo baada ya kuwa Mkenya wa kwanza kufunga bao kwenye ligi ya Uhispania Laliga.
Aidha, Olunga almaarufu “Engineer ” amekuwa mchezaji wa kwanza wa klabu hiyo ya Girona kufunga mabao matatu kwenye mechi moja.
Itakumbukwa kuwa Olunga alijiunga na Girona kutoka klabu ya Guizhou Zhicheng ya Uchina mwaka jana. Msimu wa kwanza kwa Olunga haukuwa mwema kwani hakuchezeshwa kwenye kikosi cha kwanza.
Hata hivyo, mwaka huu wa 2018 umeanza vyema kwa Mkenya huyo ambaye amefunga mabao matatu na kuisaidia Girona kuirindima Las Palmas mabao sita kwa nunge.
Girona ilipata bao lake la kwanza kupitia kwa Stuani dakika ya ishirini na tano kwa njia ya penalti. Kipindi hicho cha kwanza kilikamilika kwa bao hilo moja, huku Olunga akiingia kama nguvu mpya kipindi cha pili na kuleta msisimko wa aina yake.
Mhandisi huyo alipata bao lake la kwanza dakika ya hamsini na saba, kabla ya kucheka na wavu dakika ya sabini kwa mara nyingine. Ni wazi kuwa Olunga alikuwa hajakamilisha shughuli yake kwani alifunga la tatu dakika ya sabini na tisa na kuacha mashabiki vinywa wazi.
Wachezaji wa Girona walionekana kuwa na uhodari wa kipekee kwani Garcia alifunga bao dakika ya sitini na nne, kabla ya Portu kuingia kwenye orodha ya wafungaji kwa bao dakika ya sabini na nne.
Mabao hayo sita na ushindi huo umeiacha Girona kwenye nafasi ya tisa, katika jedwali la Laliga.
Bila shaka ni furaha iliyoje kwa Wakenya kuona kijana wao akiipeperusha bendera ya Kenya Uhispania.