Mshambulizi wa Kariobangi Sharks na timu ya taifa Harambee Stars, Masoud Juma amejiunga na klabu ya Afrika Kusini Cape Town City. Klabu hiyo ilitangaza usajili huo katika mtandao wao wa Twitter mapema leo. Hata hivyo hela za usajili hazijawekwa wazi.

 

Juma amekuwa nguzo muhimu kwa kikosi cha Harambee Stars kilichotwaa taji la CECAFA Desemba ya mwaka 2017, huku akifunga mabao mawili. Nyota huyo alifunga bao kwenye mechi ya kwanza dhidi ya Rwanda na kupata jeraha kabla ya mechi hiyo kukamilika.

Jeraha hilo lilimweka nje kwa mechi zilizofuata lakini akapata afueni na kucheza kwenye fainali. Juma aliingia kama nguvu mpya dhidi ya Zanzibar na kufunga bao maridadi dakika za nyongeza. Harambee Stars ilipata ushindi muhimu kwenye kipute hicho baada ya mlindalango Patrick Matasi kuokoa mikwaju mitatu ya penalti za Wanazanzibar.

 

HISTORIA YA MASOUD JUMA

Taaluma ya nyota huyu ilianzia shule ya Sekondari kule Isiolo Barracks alipoiwakilisha shule hiyo kwenye michuano ya Coca Cola, alipoibuka mfungaji bora kwa mabao matano. Juma pia alitajwa kama mchezaji bora wa kipute hicho.

Baadaye Juma alisajiliwa na timu ya Kiambaka Christian Centre (KCC) kule Meru, inayoshiriki ligi ya Divisheni ya Kwanza. Mkufunzi wa KCC George Maina alimnoa Juma na haikuchukua muda kabla ya mshambulizi huyo kujiunga na klabu ya Shabana.

Kule Shabana, Juma alijijengea jina pamoja na Cornelius Juma, huku mkurugenzi mkuu wa Shabana Gilbert Selebwa akimlinganisha Masoud na aliyekuwa nyota wa Harambee Stars, Dennis Oliech.

Juni mwaka wa 2014, Masoud alijiunga na klabu ya Bandari kutoka Pwani na inayoshiriki ligi kuu KPL.  Hata hivyo, haikuwa rahisi kwa Juma kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza, na ilimbidi atie bidii maradufu.

Juma pamoja na wenzake,Victor Ndinya, Fareed Mohammed, Khamis Tole na David King’atua waliipeperusha bendera ya Bandari kwa takriban miaka miwili. Kwa bahati mbaya, Juma alipata jeraha baya lililomweka mkekani kwa miezi sita.

 

Mwezi Septemba 2016, Juma alirejea mazoezini na kushiriki kwenye kipute cha Shield Cup huku akifunga bao la nne kwenye fainali, ambapo Bandari iliilaza Nakumatt mabao manne kwa mawili.

 

Baada ya ufanisi huo, Juma alihamia Sony Sugar alikocheza kwa mwaka mmoja kabla ya kusajiliwa na Kariobangi Sharks. Mchezaji huyo aliisaidia Sharks kumaliza kwenye nafasi ya sita kwenye KPL msimu wa 2017, huku wakitwaa taji la GoTV Shield Cup.

Juma alishinda tuzo la mfungaji bora wa Ligi kuu msimu wa 2017, huku akiwapiku Vincent Oburu na Meddie Kagere.

 

Nyota huyo atajiunga na Cape Town City ambapo atalenga kuzidi kufunga mabao. Bila shaka namtakia kila la heri.

Leave a Comment