MASAIBU YA SUMGONG
Bingwa wa mbio za masafa marefu, Jemima Sumgong amepigwa marufuku ya miaka nne. Sumgong alivunja rekodi ya dunia mwaka jana kule Brazil ( Rio Olympics 2016)alipomaliza wa kwanza na kutwaa dhahabu kwa Kenya.
Taarifa za kumhusisha na matumizi ya dawa za kusisimua misuli ziliibuliwa baada ya ushindi huo, madai aliyoyakana Sumgong. Hata hivyo, shirikisho la riadha duniani IAAF kwa ushirikiano na WADA; shirika linalochunguza matumizi ya dawa hizo haramu, liliamua kumfanyia vipimo.
Vipimo vya kwanza aina ya “A” vinavyohusu damu kukaguliwa vilitokea chanya, kudhihirisha wazi kuwa Sumgong alikuwa anatumia dawa haramu. Hata hivyo, sharti mwanariadha apimwe mara mbili ili kuhakikisha ukweli wa vipimo hivyo.
Hii Leo, Novemba saba vipimo vya pili aina ya “B” vimekuwa chanya kudhihirisha wazi kuwa Sumgong amejishindia medali kadha kwa usaidizi wa dawa za kusisimua misuli.
Sheria za IAAF zinamkubalia mwanariadha huyo kukata rufaa dhidi ya marufuku hiyo.
Mpenzi msomaji fahamu kuwa Sumgong hufunzwa na mumewe Noah Talam, ambaye humwongoza mazoezini huko Nandi chini ya kocha mkuu Dkt. Gabriel Rosa.
Itakumbukwa kuwa Talam ni kakaye Sarah Chepchirchir, mwanadada aliyeshinda mbio za Tokyo, Februari mwaka huu. Hili ni onyesho dhahiri kuwa haikuwa rahisi kumshuku Sumgong.
Mwaka wa 2014, Rita Jeptoo alipigwa marufuku ya kutoshiriki riadha,baada ya kupatikana na chembechembe za dawa hizo haramu na kujiunga na wenzake waliotemwa awali. Rita alinyakua dhahabu kwa kushinda mbio za Chicago na Boston mwaka huo.
Kinachoshtua zaidi ni kuwa, Rita na Sumgong walikuwa wanafunzi wa Talam ( mumewe Sumgong) ingawa kocha mkuu wa Rita alikuwa Claudio Beradelli. Baada ya matokeo hayo, Claudio alikana kuhusika huku akisema kuwa Rita alitumia dawa kisiri.
Inasubiriwa kujulikana ikiwa Sumgong atakataa rufaa dhidi ya uamuzi wa IAAF, na ikiwa kocha wake Gabriel Rosa atakana kuhusika.
Swali kuu ni je, kama kocha utakosaje kujua mwanafunzi wako anatumia dawa za kusisimua misuli na mko naye mazoezini mara mbili kwa siku? Akili kichwani.