GHANA 5-0 KENYA

PAULINE ADOBEA ALIFUNGA MABAO MANNE

Kwa kweli, hakuna zuri lisilo kuwa na mwisho. Msururu wa matokeo mazuri ya Harambee Starlets ulifika mwisho hapo jana, baada ya kurindimwa mabao matano kwa nunge na mabinti wa Ghana kule Accra.

Kocha wa Ghana Yussif Basigi alimwanzisha Martha Annano kama mlindalango naye Justice Tweneboah akashirikiana na Gladys Amfobea, Blessing Agbomadzi na Felicity Asuaku kwenye ulinzi.

Grace Asantewa, Helena Obeng, Oliver Anokye na Rafia Kulchiri walikuwa viungo wa kati huku Pauline Adobea na Sandra Owusu Ansah wakishambulia.

Helena Obeng alifungua karamu ya mabao dakika ya nane huku Adobea akifunga mawili dakika za thelathini na tano na arobaini na nne.

Adobea alikuwa na kazi rahisi kuwakebehi na kuwadhalilisha walinzi wa Starlets kwani walifanya makosa hapa na pale. Bao la tatu lilianzishwa na mlinzi wa Starlets kwa kupiga pasi mbovu iliyompata mpinzani.

Black Princesses wa Ghana

Anokye, Asantewaa na Obeng walipoteza nafasi kadhaa kipindi cha pili katika juhudi za kupata bao la nne. Hata hivyo, Adobea aliyekuwa amewasoma walinzi wa Starlets alifunga bao la nne dakika ya hamsini na tisa kabla ya kucheka na wavu dakika ya sabini na sita.

Starlets watakuwa na kibarua cha kushuka mchongoma watakapoalika Black Princesses Nairobi kwenye marudio ya mechi hizo.

Kikosi cha Harambee Starlets

Lilian Awuor( Kipa); Foscah Nashivanda,Leah Cherotich, Lucy Akoth,Wincate Kaari,Corazon Aquino, Quinter Atieno, Diana Wacera, Martha Amunyoleto, Stella Anyango,Jentrix Shikangwa.

Leave a Comment