Mlinzi wa Southampton Virgil Van Djik atajiunga na Liverpool mwezi Januari tarehe moja kwa rekodi ya paundi milioni sabini na tano (£75M).

Nyota huyo wa Uholanzi alifaa kujiunga na The Reds mwezi Julai, ila uhamisho huo ukafeli baada ya kujulikana kuwa Liverpool haikufuata sheria katika kutaka kumsajili.

Usajili huo wa Van Djik utakuwa ghali zaidi huku akimpiku Benjamin Mendy wa Manchester City, aliyesajiliwa kwa paundi milioni hamsini na mbili (£52M) kutoka klabu ya Monaco.

Van Djik mwenye umri wa miaka ishirini na sita, amesema kuwa anafurahia kujiunga na mojawapo ya klabu kubwa duniani. Aidha, Djik amekiri kuwa na wakati mgumu kule St Mary’s.

Mlinzi huyo aliachwa nje ya kikosi cha Southampton kilichocharazwa na Tottenham mabao matano kwa mawili Jumamosi, hivyo kuzidisha fununu kuwa angeondoka.

 

Van Djik alijiunga na Southampton mwaka wa 2015 kutoka klabu ya Celtic kwa paundi milioni kumi na tatu (£13M), na alitia sahii ya miaka sita mwaka jana na klabu hiyo ya kusini kwa Uingereza.

 

Baada ya miamba wa Uingereza Liverpool kutaka kumsajili, nyota huyo aliwasilisha ombi la kutaka kuondoka jambo lililomfanya kocha wake kumtema mazoezini huku Djik akilazimika kufanya mazoezi peke yake.

Hata hivyo kocha wake Mauricio Pellegrino alimrejesha kwenye kikosi cha kwanza mwezi Septemba dhidi ya Crystal Palace, mechi ambayo Southampton ilitwaa ushindi.

 

Klabu yake ya zamani ;Celtic itanufaika kwa usajili huo kwani klabu hiyo ilikuwa na maelewano ya asilimia kumi na Southampton ikiwa nyota huyo angeuzwa baadaye.

 

Licha ya kujiunga na Liverpool tarehe moja, Djik hataweza kushiriki kwenye mechi ya siku hiyo dhidi ya Burnley, kwani usajili wake utakamilika rasmi tarehe mbili.

Liverpool imetangaza kuwa Djik atavaa jezi nambari nne. Mlinzi huyo ameweza kupita usajili wa Naby Keita  kutoka RB Leipzig, kiungo anayetarajiwa kujiunga na Liverpool vilevile mwaka ujao Juni.

Van Djik ndiye mchezaji wa sita kujiunga na Liverpool kutoka Southampton. Wengine ni Sadio Mane (£34M), Adam Lallana (£25M), Dejan Lovren (£20M), Nathaniel Clyne (£12.5M) na Rickie Lambert ( £5M).

 

Leave a Comment