Kayumba Soter alivyomtega Jockins Atudo

 

Timu ya taifa, Harambee Stars inashikilia uongozi wa Kundi A kwenye mechi zinazoendelea za CECAFA, baada ya kuinyuka Rwanda mabao mawili kwa nunge. Mechi hiyo ambayo ilifungua michuano hiyo rasmi, ilisakatwa kule Kakamega, kwenye uga wa Bukhungu.

 

Masoud Juma aliipa Kenya bao la kwanza dakika ya ishirini na tano kabla ya Duncan Otieno kucheka na wavu dakika kumi na mbili baadaye. Bao la Duncan lilikuwa stadi mno kwani aliweza kuinua fataki hiyo kutoka katikati mwa uwanja.

 

Timu zote zilipoteza nafasi kadha za wazi ila ilikuwa uchungu mno kwa upande wa Rwanda, kwani walishindwa kupata angaa la kufutia machozi. Kipindi cha pili kilijawa na mhemko si haba huku mlinzi wa Rwanda Kayumba Soter akipata kadi nyekundu, dakika ya sabini na mbili.

 

Abdul Faissal, Nahodha wa Libya ( jezi 18; kushoto), akijaribu kumkaba mshambulizi wa Tanzania.

Katika mechi nyingine ya Kundi hilo, Tanzania waliambulia sare tasa dhidi ya Libya, mechi iliyochezewa kule Kenyatta Stadium, Machakos.

Timu hizo zilishambulia kwa kiwango sawa vipindi vyote,huku Mbaraka Yusuph na Yahya Zaid wa Kilimanjaro Stars wakipoteza nafasi za wazi. Hata hivyo, heko ni kwa walinzi wa Libya na nahodha wao Abdul Faissal waliohakikisha ukuta unasimama tisti.

 

Jumatatu ya tarehe nne, Uganda waliambulia sare tasa dhidi ya Burundi, mechi iliyogaragazwa kwenye uga wa Kenyatta, kule Machakos. Mshambulizi wa Burundi Fiston Abdoul alipoteza nafasi nyingi mno, hongera kwa kipa wa Uganda na walinzi wake.

Uganda Cranes walimiliki mchezo huo kwa asilimia sabini lakini hawakufaulu kupata bao.

Leave a Comment