Vijana wa Marshalls waachiwa kivumbi na wazee waliosheheni uzoefu katika debi ya “funga-nifunge”

Hali ilikuwa si hali Jumamosi ya tarehe tatu pale Pavilion, baada ya mibabe wa zamani kuwafunza kandanda vijana chipukizi wa Marshalls. Kipute hicho kilichosubiriwa kwa hamu na hamumu, kilishuhudia halaiki ya mashabiki kutoka bewa kuu la Chuo Kikuu cha Moi, na maeneo jirani.

Vijana wa nyumbani walikuwa wa kwanza kuchokoza nyuki, walipofunga bao dakika ya tano, kupitia kwa Eugene Kwasima. Hii ilikuwa baada ya pasi za uhakika kutengenezwa pale katikati na Job Omariba kwa ushirikiano na Chris Wasike, hivyo kusababisha bao la kupigiwa mfano.

Hata hivyo, uongozi wa chipukizi hao haukudumu kwa muda mrefu, kwani Evanso alisawazishia wazee wa kazi kunako dakika ya kumi na tatu. Mibabe hao walijipanga vilivyo huku mipira yote mizuri ikipikwa na Augustine Gutta almaarufu “Ucho” kwenye kiungo. Ucho alikuwa mwepesi huku maarifa yake yakitengeneza nafasi kadha licha ya nyingine kuambulia patupu.

Umiliki wa mpira kwenye robo ya pili ya mechi uliegemea mashujaa hao, waliochezea Marshalls enzi zao chuoni Moi. Krosi za chipukizi wa nyumbani zilikatwa kirahisi huku pasi zao zikikosa kufika.

Ukakamavu huo wa mashujaa uliwatunuku bao la pili dakika ya ishirini na moja, Evanso alipomzidi maarifa mlinzi Morris Kweyu “OCS” na kumpa Keith pasi maridadi aliyoigeuza bao , na kumwacha kipa Kevin Omondi hoi.

Kikosi cha mashujaa almaarufu “Legends”

 

Mashujaa waliwapa vijana hao shinikizo si haba huku kipa Kevin akiokoa mikiki kadha ya hatari. Juhudi za watoto wa nyumbani kuregegea kwenye mechi ziligonga mwamba, huku kipindi cha kwanza kikikamilika Mashujaa kifuambele.

Kipindi cha pili kilisheheni mabadiliko machache kwenye vikosi vyote. Arthur Watenda alichukua nafasi ya Makachia Kevin huku Ucho pia akipumzishwa baada ya kuumia. Upande wa machipukizi, Arnold Omwongo aliingia kama nguvu mpya pamoja na Michael Kariuki.

Kuingia kwa Arnold kuliipa timu ya machipukizi wa Marshalls msisimko wa aina yake, kwani kijana huyo alionyesha kujiamini kwa kipekee huku akitengeneza nafasi kadhaa. Ama kwa kweli, atafutaye hachoki, vijana hawa walipata bao la pili na la kusawazisha baada ya Shiveka Shadrach “Anguilla” kuwapita walinzi Methae Odunga na Chinjili na kupiga shuti nzito lililotiwa kimiani na Daniel Makolo. Kipa Charles Brian alibaki akigagaa nyasini kwani alikuwa amekwishachelewa kufika.

Sehemu iliyosalia ya kipindi hicho ilishuhudia utafutaji wa mabao, ambao haukufanikiwa huku Mashujaa wakishindwa kusababisha hatari kwa kumkosa Ucho. Mechi hiyo ilikamilika kwa sare hiyo ya mabao mawili.

Mechi iliyofuata, Kocha wa vijana wa Marshalls Alphonce Juma alitumia kipa Kevin Omondi tena, madifenda Chege, Victor, Eric na “Cobra”. Kiungo cha kati kilisheheni Ologi na Phelo, huku ubavu wa kulia ukihusu David Kasyoki na ule wa kushoto ukichezwa na Otto.

Vijana chipukizi wa Field Marshalls pamoja na kocha wao; Alphonce

 

Mashambulizi ya kikosi hicho yalifanywa na Federico Muia. Wazee wa kazi walimwanzisha kipa Charles kwa mara nyingine, John Mbati, Martin Nyati, José, Guti, Evanso , David na Methan Odunga.

Mechi hiyo ilikosa kuzalisha mabao kwani vikosi vyote vilionekana kukomaa. Walinzi wa mashujaa hawakuwapa nafasi Muia na Kasyoki kushambulia huku, Phelo na Victor wakiwakaba Kevin Makachia na Evanso. Kipindi cha kwanza kilikamilika kwa sare tasa.

Kwenye kipindi cha pili, kocha Alphonce aliwapumzisha Muia na Kasyoki huku Don na Mohameed wakiingia kwenye mashambulizi. Hata hivyo, shuti zao hazikulenga lango wala kusababisha hatari kwani walinzi wa mashujaa walikuwa macho kabisa kuondoa hatari hiyo.

Kwa mara nyingine, uzoefu ulikosekana kwenye kikosi cha machipukizi walipomtega mshambulizi wa mashujaa kwenye kijisanduku na kusababisha penalti.

Kocha Alphonce akiwapa vijana wake mawaidha

Jukumu la upigaji lilitwikwa José ambaye hakubahatisha, bali alitia mpira ndani ya wavu. Kipa Kevin Omondi alijaribu kuufwata mpira huo aliokuwa ameuona vyema, lakini hakufanikiwa. Bao hilo moja lilisimama hadi kipenga cha mwisho, huku mashujaa wakitoka kwa mbwembwe za kipekee.

Leave a Comment