Dereva wa Ferrari Sebastian Vettel ndiye bingwa wa mbio za langalanga; Grand Prix zilizoandaliwa kule Brazil. Bingwa huyo alimpiku Valtteri Bottas huku dereva nambari moja duniani, Lewis Hamilton akimaliza nafasi ya nne.
Katika dakika muhimu, Vettel alimpita Bottas kwenye kijia maalum, huku akiingia kwenye kona ya kwanza na kisha kujitokeza mbele ya dereva huyo wa Mercedes. Juhudi za Bottas kurejea uongozini zilifeli.
Ushindi huo ni wa arobaini na saba kwa Mjerumani huyo na wa kwanza tangu mwezi Julai. Vettel alionyesha dalili za kushinda mbio hizo tangu mwanzo, kwani hakuruhusu Bottas kumpita kwa hata sekunde mbili kabla ya mbio kukamilika.
“Dalili zote zilionyesha kuwa angeshinda”, alisema Martin Brundle, mwanahabari wa mbio hizo kwenye kituo cha Sky Sports. Vettel sasa anashikilia nafasi ya pili duniani, nyuma ya Hamilton huku Bottas akichukua nafasi ya tatu.Ushindi huo pia ni watatu kwa Vettel kwenye taaluma yake huko Interlagos.
Daniel Ricciardo alimaliza wa sita; nafasi moja nyuma ya dereva mwenza Max Verstappen. Ricciardo alikuwa amekwama awali mbio zilipoanza lakini kumaliza katika nafasi hiyo ilikuwa afueni si haba.
Dereva huyo kutoka Australia, alishuhudia gari lake likigeuzwa kijimpira, na kubingiria baada ya kugongana na Stoffel Vandoorne na Kevin Magnussen, ambao hawakumaliza mbio hizo.
Ricciardo alirejea baadaye baada ya kuhudumiwa, huku akipinda mbele ya magari kadhaa na kusonga hadi nafasi ya sita.
Mbio hizo zilizidi kuibua msisimko kwani Lewis Hamilton alijipata taabani pia alipogongana na Kimi Raikkonen katika mkwaruzano wa kumaliza kwenye nne bora.
Awali Hamilton alikuwa ameongoza mbio hizo, kwani kasi yake ilikuwa ya kupigiwa mfano. Bingwa huyo wa Dunia alishikilia uongozi hadi nusu ya mbio nzima, kabla ya kukatizwa ghafla na Raikkonen sekunde chache baada ya kumpita Verstappen.
Ikiwa angempita Raikkonen, Hamilton angeshinda mbio hizo na kuandikisha rekodi mpya, kwani Bottas alikuwa mbele yake kwa mita chache.Hamilton alilazimika kutosheka na nafasi ya nne huku akipokea tuzo la Dereva wa Siku.
“Tulipoteza mbio hizo katika kona ya kwanza ” alijuta Bottas. Dereva huyo aliyemaliza wa pili, alikuwa ametishia kumpiku Vettel lakini Mercedes ilikuwa imemwita asimame na Vettel alichukua nafasi hiyo kumpita zaidi.
Vettel hakuthubutu kuachwa nyuma kwa zaidi ya sekunde mbili kwenye raundi ishirini za mwisho na hatimaye aliibuka mshindi.
“Ni matokeo mazuri.Imekuwa siku ndefu yenye ushindani mkali. Sisi sote tulikuwa na kasi sawa hivyo hapakuwa na nafasi ya kufanya makosa”, alisema Vettel.
Vettel na Bottas, wanaoshikilia nafasi za pili na tatu duniani mtawalia, watakuwa na fursa ya kujiboresha katika mashindano ya Abu Dhabi Grand Prix, wiki mbili zijazo.
MASSA ASTAAFU KISHUJAA
Katika kilele cha kusisimua, nyota wa F1 Mbrazili Felipe Massa alimaliza nafasi ya saba katika kuwaaga mashabiki. Massa alikumbwa na upinzani mkali kutoka kwa Fernando Alonso ambaye waliwahi hudumia Ferrari pamoja.
Sergio Perez alikuwa amewakaribia na akavuka kijia chini ya sekunde moja, kabla ya Massa kupigiwa makofi na mashabiki, huku mwanawe akimpongeza kupitia kwa redio ya timu yake.
Massa aliwashukuru mashabiki wake wa Interlagos, huku akiwaaga kwa machozi.
“Najihisi mshindi leo”, alisema dereva huyo ambaye atastaafu mwishoni mwa msimu.
Fernando Alonso aliyemaliza wa nane, alimpongeza Massa huku dereva huyo wa McLaren akiwaahidi mashabiki wake mazuri. ” Mwaka ujao utakuwa bora zaidi”, alisema Alonso.
1 Comment