Miamba wa Laliga Uhispania, Barcelona wamefanikiwa kumpata Philippe Coutinho kutoka Liverpool kwa rekodi ya Euro milioni mia moja sitini (€100M).

Barca wamempata nyota huyo baada ya muda mrefu wa kutuma maombi yaliyokataliwa. Kipindi kilichopita cha uhamisho, kilishuhudia uhamisho wa Coutinho ukigonga mwamba dakika za lala salama, baada ya Liverpool kusema nyota huyo hakuwa wa kuuzwa.

 

Coutinho anatarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya baadaye Leo na atahudhuria mechi ya Barcelona dhidi ya Levante. Klabu hiyo inatumai kuwa nyota huyo atashiriki mazoezi na wachezaji wa klabu yake mpya, Jumatatu.

 

Barcelona italipa Euro milioni mia moja ishirini (€120 M) kama ada ya kwanza, huku Euro milioni arobaini (€40M) zikilipwa baadaye kulingana na mchango wa Coutinho kwa timu hiyo na mechi atakazoshiriki.

 

Baada ya uhamisho huo, Coutinho sasa ni mchezaji wa tatu kwenye orodha ya wachezaji ghali, baada ya Neymar Jr (€220M) na Kylian Mbappe (€180 M) wote wa Paris Saint Germain.

 

Nyota huyo kutoka Brazili ndiye mchezaji ghali zaidi kwa timu ya Barcelona baada ya kuvunja rekodi ya Ousmane Dembele (€105M), na kutoka timu ya Uingereza kwa kumpiku Paul Pogba (€105M).

 

Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp amewaambia mashabiki wa klabu hiyo kuwa walifanya kila wawezalo kumsihi Coutinho kusalia na timu hiyo, ila akakataa. Klopp amesema kuwa Coutinho alitaka sana kujiunga na Barcelona huku akidai ilikuwa ndoto yake kuchezea timu hiyo.

Sasa inasubiriwa kuona Liverpool watasajili nani kujaza nafasi iliyoachwa na Coutinho.

Leave a Comment