Kiungo wa Arsenal na timu ya taifa ya Nigeria, Alex Iwobi ameandikisha historia kwa kufunga bao muhimu na kuhakikisha miamba hao wanafika Urusi mwaka ujao.

Nyota huyo alifunga bao hilo dakika ya sabini na mbili kwenye kipindi cha lala salama baada ya mabeki wa Zambia kukosa umakinifu. Mechi hiyo ilizua mchecheto si haba vipindi vyote viwili na sare ilikuwa dhahiri kabla ya Iwobi kukamilisha krosi ya Abraham Shehu na kumwacha kipa wa Zambia, Kennedy hoi.

Kwingineko, Afrika Kusini iliinyanyasa Burkina Faso mabao matatu kwa moja katika mechi ya awali na kufuzu kwa Kombe la Dunia. Percy Tau alifungua ukurasa wa mabao kwa Bafana Bafana, Themba Zwane akafunga la pili kabla ya Vilakazi kutia la tatu dakika ya arobaini na sita. Alain Traore aliifungia Burkina Faso la kufutia machozi dakika ya themanini na saba kwa kukunja mkwaju wa adhabu hadi nyavuni.

Cameroon  iliilaza Algeria mawili kwa nunge huku Uganda ikitoka sare ya kutofungana na Ghana. Katika mechi nyingine,  Tunisia iliilaza Guinea manne kwa moja, Senegal ikailemea Cape Verde mawili kwa bila nayo DR Congo ikiichabanga Libya mawili kwa moja.

Awamu ya nne ya mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia itaandaliwa mwezi Novemba mwaka huu.   

Yassina Terry

Alex Iwobi

 

Leave a Comment