- KIDUMBWEDUMBWE:TUZO ZA FIFA 2017
Naam, hayawi hayawi huwa, tuzo zilizosubiriwa kwa hamu na hamumu na mashabiki wapenzi wa soka ulimwenguni, ziliandaliwa hiyo jana kule London, Uingereza. Kama ilivyotarajiwa, Cristiano Ronaldo alitwaa tuzo la mchezaji bora duniani kwa wanaume huku Lieke Martens akitajwa mwanasoka bora kwa kina dada.
Baada ya msimu wa kuridhisha kule Real Madrid na kwenye timu ya taifa ya Ureno, Ronaldo alitwaa tuzo hilo la Ballon D’OR kwa mara ya tano mfululizo katika taaluma yake. Ronaldo almaarufu “Cr7” aliisaidia Real Madrid kutetea na kuhifadhi kombe la Mabingwa huku taifa lake likifika kwenye nusu fainali ya michuano ya mabara yaani, FIFA Confederations Cup.
Ronaldo alitwaa asilimia arobaini na tatu ya kura zilizopigwa, Lionel Messi akipata asilimia kumi na tisa huku Neymar JR akitwaa asilimia sita ya kura zote.
Mwanadada, Lieke Martens mwenye umri wa miaka ishirini na nne, alitwaa asilimia ishirini na moja ya kura zote huku akiwapiku Carli Loyd na Deyna Castellans wal’oibuka wa pili na tatu mtawalia. Makocha wa Cristiano Ronaldo na Lieke Martens; Zinedine Zidane na Sarina Wiegman walituzwa kuwa makocha bora ulimwenguni kwa wanaume na wanawake mtawalia.
- TUZO ZA BINAFSI
Kipa Bora : Gianluigi Buffon; Juventus
Buffon aliisaidia Juventus kufika fainali ya kombe la Mabingwa walipopoteza kwa Real Madrid. Kipa huyo wa timu ya taifa ya Italia, alitajwa kama kipa wa timu bora ya FIFA almaarufu FIFA FIFPRO WORLD11.
Bao bora la mwaka ; Olivier Giroud , Arsenal
Tuzo hilo lijulikanalo kama FIFA Puskas Award lilimwendea Mshambulizi wa Arsenal na timu ya taifa ya Ufaransa, Olivier Giroud baada ya bao lake la kumezewa mate dhidi ya Crystal Palace. Giroud alifunga bao hilo kwa mtindo wa nge “scorpion kick”, kwenye mechi hiyo iliyosakatwa kwenye mkesha wa mwaka mpya, Januari mwaka huu.
Tuzo la mchezo mwema: Francis Kone, Senegal
Tuzo hilo lijulikanalo kama “ FIFA Fair Play Award” lilituzwa Francis Kone kutoka Senegal baada ya kuokoa maisha ya mchezaji wa timu pinzani. Kone alimfanyia huduma ya kwanza Kipa wa Bohemians 1905 kwa jina Martin Berkovec katika ligi ya Jamhuri ya Czech.
Tuzo la Mashabiki : Mashabiki wa Celtic FC
Mashabiki wa klabu ya Celtic kutoka Scotland walitajwa kuwa bora zaidi ulimwenguni kwa bidii yao na kujituma katika kushabikia timu hiyo. Mashabiki hao walipata asilimia hamsini na tano ya kura baada ya kutengeneza kadi ya digrii mia tatu sitini (360℅) katika mechi ya mwisho kwenye ligi msimu Jana, katika ukumbusho wa miaka hamsini walipotwaa kombe la bara Uropa mwaka wa 1967.
Timu bora ya FIFA : FIFPRO WORLD11
Kipa: Gianluigi Buffon
Walinzi: Dani Alves, Leonardo Bonucci, Marcelo, Sergio Ramos
Viungo: Andres Iniesta, Luka Modric, Toni Kroos
Washambulizi: Cristiano Ronaldo, Lionel Messi, Neymar Jr
