Mechi za kufuzu , Kombe la Dunia kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka ishirini zitang’oa nanga mwezi huu wa Novemba. Timu ya taifa Harambee Starlets imeratibiwa kucheza na Ghana, Jumapili ya tarehe tano kwenye uga wa Cape Coast Stadium, kule Accra.
Timu hiyo ya wanadada wachanga, imekuwa ikipiga mazoezi kwa zaidi ya wiki kule Kenyatta Stadium Machakos, katika matayarisho ya mechi hizi. Hata hivyo, ni wachezaji kumi na saba pekee waliojitokeza kambini kati ya thelathini waliotarajiwa. Miongoni mwa waliokosa, saba wanafanya mitihani ya kitaifa kwa kidato cha nne, KSCE ambao ni; Sheryl Angachi, Cynthia Shilwatso, Maureen Khakasa, Cynthia Akinyi na Sharon Adhiambo.
Oktoba mwaka huu, Harambee Starlets ilitoka sare ya mabao mawili dhidi ya Ethiopia kule Addis Ababa, kabla ya kucharaza wajukuu hao wa Haile Selassie mabao mawili kwa moja, kule Machakos. Ushindi huo uliisaidia Starlets kufuzu kwa awamu ya pili ya mechi hizo, kwani walikuwa na jumla ya mabao manne dhidi ya yale matatu ya Ethiopia.
Kina dada hao watakuwa na kibarua kigumu dhidi ya Ghana wikendi hii, kwani ndiyo timu pekee iliyovuna ushindi mnono, kwenye awamu ya kwanza. Ghana iliirindima Algeria mabao kumi kwa nunge kwenye mikondo yote huku wakifunga mabao matano kila mechi; nyumbani na ugenini. Wawili hao watakutana kwenye marudiano wikendi ya tarehe kumi na nane na kumi na tisa, mwezi huu.
Mshindi kati ya Ghana na Kenya atafuzu kwa awamu ya tatu na ya mwisho itakayoandaliwa mwezi Januari mwakani. Bara la Afrika limetunukiwa nafasi mbili kwenye Kombe la Dunia mwakani, kwa wanadada chipukizi wasiozidi miaka ishirini, litakaloandaliwa Paris, Ufaransa.