
Beki mstaarabu Laurent Koscielny atastaafu toka soka la kimataifa baada ya Kombe la Dunia mwaka ujao, kule Urusi. Koscielny ameichezea Les Bleus mechi arobaini na tisa na itakumbukwa kuwa alicheza mechi yake ya kwanza mwaka wa 2011, Ufaransa dhidi ya Marekani.
Akizungumza na kituo cha L’Equipe, Koscielny alisema; ” kuna mwisho wa kila jambo. Baada ya kombe la dunia, nitakuwa nimetimu miaka thelathini na tatu, na utakuwa wakati murua wa kutundika daluga.”
Mlinzi huyo mwenye umri wa miaka thelathini na mbili, ameichezea Ufaransa kwa dimba tatu kuu, na alikuwa kwenye kikosi kilichomaliza cha pili, Euro 2016. Beki huyo anastaafu ili aweze kuichezea Arsenal zaidi.
Koscielny amekuwa na majeraha kadhaa ya kifundo cha mguu( ankle) na inabidi atibiwe kila siku. “Kila siku mie natibiwa jeraha hili na najua nitafanya hivyo hadi mwisho wa taaluma yangu.” Alisema mlinzi huyo.
“Sasa, nafanya hivyo kila siku na ni sawa ila wakati mwingine si rahisi kwani tunacheza siku tatu kwa wiki. Nahitaji kupumzika ili jeraha hili lipone kabisa,” alisema Koscielny.
