MISRI YAFUZU HUKU MOROCCO IKIIZIMA IVORY COAST

Wachezaji wa Tunisia baada ya kufuzu

Bao la Edwin Gyasi lilisaidia Black Stars kuokota alama moja dhidi ya Misri katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia, Jumapili. Wajukuu hao wa Firauni walikuwa wa kwanza kufuzu walipopata ushindi mkubwa dhidi ya Congo-Brazzaville, mwezi Septemba.

Misri ilipata uongozi wa mechi hiyo dakika ya sitini na moja kupitia kwa Shikabala, baada ya kuunganisha krosi ya Trezeguet. Kiki lake, alilochonga kwa mguu wa kushoto lilimwacha Richard Ofori hoi, na kuacha wavu ukitingika.

Awali, Wakaso Mubarak alikuwa amemlazimu kipa Sherif Ekramy kuokoa mkuki wake huku Ghana wakihisi kuwa walinyimwa penalti dakika ya ishirini, kipa wa Misri El Shaarawy alipomtega Raphael Dwamena.

Wakaso Mubarak wa Ghana

Uongozi huo haukudumu muda mrefu kwani Gyasi, mzaliwa wa Uholanzi alisawazishia Ghana dakika tatu baadaye. Mshambulizi huyo alimzidi kipa maarifa alipombabatiza beki wa Misri, kabla ya mpira kujaa wavuni. Bao hilo lilikuwa la kwanza kwenye timu ya taifa, kwa Gyasi anayechezea Aalesund FK. Mechi ya kwanza kwa chipukizi huyo ilikuwa Septemba, Black Stars ilipoirindima Congo mabao matano kwa moja.

Ghana walikuwa bila Jordan na Andre Ayew , Christian Atsu na Asamoah Gyan waliokuwa mkekani wakiuguza majeraha.Sare hiyo ilimwacha Ghana kwenye nafasi ya tatu na alama saba, sita nyuma ya Misri anayeongoza jedwali.

Katika mechi nyingine, Uganda ilitoka sare ya bao moja dhidi ya Congo kule Brazzaville, huku wakimaliza wa pili kwa alama tisa, nyuma ya Misri. Congo inashikilia mkia kwa alama mbili baada ya mechi sita. Congo ilikuwa inaongoza, Marvin Baudry alipofunga dakika ya kumi lakini Milton Karisa akasawazishia Uganda, dakika moja baadaye.

Kwingineko,Tunisia ilifuzu kwa Kombe la Dunia kwa kutoka sare tasa dhidi ya Libya. Wapinzani wao DR Congo ndio waliokuwa tisho kubwa kwao Ila sare hiyo iliwapa alama moja iliyowaweka kifua mbele, kwenye jedwali.

Mashabiki wa Tunisia

DR Congo iliilaza Guinea mabao matatu kwa moja kule Kinshasa na kujipatia alama kumi na tatu kwenye jedwali huku Tunisia wakiwashindia alama moja.

Tunisia, watashiriki Kombe la Dunia kwa Mara ya tano, na ya kwanza tangu mwaka wa 1996. Taifa hilo la kaskazini mwa Afrika linafunzwa na Nabil Maaloul, kocha ambaye aliwahi kuchezea Hannover 96, kati ya mwaka wa 1989 na 1991.

Katika kundi jingine, Morocco iliiduwaza Ivory Coast na kufuzu kwa Kombe la Dunia, huku wakijiunga na majirani wao Tunisia. Ivory coast, chini ya kocha Marc Wilmots ilihitaji ushindi nyumbani Yamoussokro, Ila makosa ya kipa wao yaliua ndoto hiyo.

Nabil Dirar alifungua ukurasa wa mabao kwa Morocco dakika ya ishirini na tano, baada ya kutuma fataki nzito iliyopita hadi wavuni.Kipa wa Ivory coast, Sylvain Gbohouo alitaraji krosi hiyo itaguswa na Khalif Boutaïb ila alishtuka kuona wavu ukitingika nyuma yake.

Medhi Benatia wa Morocco, akisherehekea bao lake la pili

Dakika tano baadaye, kipa yuyo huyo alifanya kosa tena kwa kutoka langoni mapema kuondoa kona ya Mbark Boussoufa lakini ilimfikia Medhi Benatia aliyeinua mpira na kufunga la pili. Sergi Aurier angeifungia Ivory coast ila fataki yake ilipaa juu ya mtambaa panya.

Leave a Comment