Tusemezane ukweli. Wakati mwingine shabiki haoni raha kuitazama mechi ya Harambee Stars. Wengi huwa wametabiri matokeo ya mechi na kwao kutazama timu ya taifa, ni kupoteza muda.

Ukweli ni kwamba, kikosi hicho kimeshindwa kutetea hadhi yao na ni wazi kuwa hawajui kujituma. Tatizo hili ni  kubwa mno na huenda likatuzuia kushiriki michuano ya maana siku zijazo.

Baada ya ziara ya kufedhehesha kule bara Asia, kocha Stanley Okumbi amejipata kikaangoni baada ya mashabiki kushambulia kikosi chake. Hata hivyo, tatizo kubwa kwa Okumbi ni wachezaji wasiothamini au kutambua umuhimu wa bidii.

Lawama nyingi zitaelekezwa kwa kocha huyo lakini sharti tukubali kuwa muda umewadia wa kujiuliza ikiwa hawa wachezaji wetu wanathamini jezi ya timu ya taifa. Harambee Stars wamecheza mechi nne za kirafiki bila ushindi huku ikikumbukwa kuwa mwakani Kenya itachuana na Ghana katika juhudi za kufuzu kwa Kombe la Taifa Bingwa Afrika, AFCON.

Baada ya kituko hicho cha Stars kupoteza dhidi ya Iraq, taifa lililomo kwenye vita vya uasi, na dhidi ya Thailand, taifa linaloorodheshwa chini yetu na FIFA, maswali ni mengi kuliko majibu. Huenda tukawasamehe kwa kupigwa na Iraq lakini dhidi ya Thailand, timu hiyo ilionyesha mchezo wa hali ya chini mno.

Uchungu anaopitia shabiki wa timu ya taifa ni mwingi mno. Timu hiyo imetuaibisha mara si haba na ni vyema wanasoka hao wakumbushwe kuwa Kenya haijacheza kwenye michuano ya hadhi ya juu kwa takriban miaka kumi na mitatu. Tuwakumbushe kuwa watu hucheza soka kwa lengo la kushinda na kuwa sare au kupoteza si lengo la watu wenye maono na bidii.

Harambee Stars ina mastaa kama Michael Olunga, Joakins Atudo, Clifftone Miheso , Jesse Were, David Owino na wengineo. Sharti nyota hawa wasimame na wapiganie hadhi ya timu ya taifa kama wafanyavyo vilabuni vyao.

Je, kikosi cha Harambee Stars, kinajali matokeo wanayoleta nyumbani? Iwapo wanajali, wangepigana ili kutopoteza mechi mbili mfululizo. Ni dhahiri kuwa wanafanya kinyume cha hilo.

Sharti wabadilishe tabia, watie bidii kocha Stanley Okumbi naye abadilishe mfumo na mbinu zake.

Mashabiki wa Harambee stars wasononeka katika mechi ya awali.

Yassina Terry.

Leave a Comment