Dirisha la uhamisho hapa Moi litafunguliwa rasmi Jumamosi hii, huku shughuli nzima ya uhamisho ikikamilika Alhamisi ya tarehe ishirini na tano. Harakati za usajili zitaendelezwa kutoka Ijumaa saa sita usiku na kukamilika Alhamisi ijayo, wakati sawa na huo.
Huku mkondo wa kwanza wa ligi hiyo ukielekea ukingoni, timu kadhaa zitajizatiti kuvipiga jeki vikosi vyao kama matayarisho ya awamu ya pili. Kwa sasa, vilabu vya Field Marshalls na Wayia vinapishana bega kwa bega kwenye jedwali la ‘Eastern’, huku Upper Hill na Wazee wa Kazi wakipepea kule ‘Western’.
Katika mahojiano na kocha wa timu ya Wakataji, Bwana David Mathu amesema kuwa wanalenga kusajili wachezaji wapya kipindi hiki cha uhamisho. Hata hivyo, meneja huyo amesisitiza kuwa hawatowinda wachezaji wa timu nyingine ila watalenga kuleta sura mpya. Mshambulizi wa timu hiyo, Brian Lijembe pia ametoa hisia zake vilevile, akieleza kuwa dhamira kuu ya Wakataji ni kupunguza matumizi ya dawa za kulevya miongoni mwa wanafunzi.

Tuvuke boda hadi kule Upper Hill, ambapo meneja mkuu Mukangala na kocha msaidizi Alphy Otunga wanazisaka huduma za “Yorke” kwa udi na uvumba. Akijulikana rasmi kama Vincent Okinyi, Yorke anaichezea Wasafi na ni miongoni mwa washambulizi waliotia fora kwenye awamu ya kwanza. Nyota huyo anajivunia mabao zaidi ya matatu akiwa na Wasafi, hivyo basi Upper Hill watalazimika kuvunja benki ili kumnasa.
Mastaa wengine watakaong’ang’aniwa ni Elvis Ochieng na mlindalango Isaac Mulupy. Elvis ambaye ni wa pili kwa ufungaji, atawagharimu wanaomtaka kima si haba ili kuigura Wayia. Hali kadhalika mlindalango Isaac Mulupy huenda akaelekea kule Angaza au Tedians, baada ya kutoshirikishwa kwa sana pale Sharks. Yote tisa kumi, Ijumaa ijayo tutajua rasmi nani kasajiliwa wapi.
0 Comments
Vicky booker
Vicky booker Coachez (Tedians) need to sign new goalkeeper. .and sell Baily top scorer in friendly