• Aden Marwa ni refarii wa kwanza Mkenya kuteuliwa na FIFA kusimamia mechi za Kombe la Dunia

Kwa majina kamili, Aden Range Marwa Okende ni mzaliwa wa Kehancha kule Migori. Marwa mwenye umri wa miaka 41, alikuwa Mkenya wa kwanza kuhusishwa kwenye kipute cha FIFA aliposimamia Kombe La Dunia la vijana wasiozidi umri wa miaka kumi na saba, mwaka wa 2011.Refarii huyo ni mwalimu wa Hisabati na Kemia katika shule ya upili ya Kamotobo iliyoko Kaunti ya Migori.

Marwa aliteuliwa kuwa refarii msaidizi mwaka wa 2012,2013 na 2015 katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika almaarufu AFCON. Hata hivyo, itakumbukwa kuwa kazi yake ya kwanza ya kimataifa kama refarii ilikuwa mwaka wa 2000, aliposimamia mechi ya Kombe la AFCON kule Zanzibar. Baadaye FIFA ilimteua rasmi na amekuwa refarii wa kimataifa tangu mwaka wa 2011.

Mwalimu huyo ambaye amekuza taaluma yake ya urefarii kutoka chini kabisa, ni kielelezo bora cha umuhimu wa kungoja. Katika Kombe la Dunia la 2014 kule Brazil, Marwa aliitwa kusimamia mechi hizo ingawa alikuwa refarii wa hifadhi. Hata hivyo, mwaka wa 2016 alisimamia mechi za Kombe la Dunia kwa vilabu ( Club World Cup) kama refarii msaidizi.

Fauka ya hayo, Marwa alijumuishwa kwenye orodha ya marefarii wasaidizi wa Shirikisho la kabumbu Afrika CAF. Mkenya huyo pia aliteuliwa kusimamia mechi za Kombe la mashirikisho (FIFA Confederations Cup) mwaka wa 2017. Katika michuano hiyo, Marwa alihudumu pamoja na Bakary Gassama, Jean Claude Birumushuhu na Malang Diedhiou.

Kandanda ya Kenya imekumbwa na masaibu yasiyo kifani kutoka siasa duni hadi ukosefu wa vifaa murua vya kuinua hadhi ya mchezo huo nchini. Hata hivyo, uteuzi wa Marwa umeleta mwanga wa matumaini kwenye nyoyo za wachezaji na mashabiki nchini na miungu ya soka inamtakia kila la heri.

Leave a Comment