Luka Modric

Kwa mara nyingine tena, Luka Modric aliwabwaga Cristiano Ronaldo na Mohamed Salah kwa kushinda taji la mchezaji bora mwaka huu, kwa hisani ya FIFA. Modric ambaye amekuwa na mwaka wa fanaka, alishinda taji la mchezaji bora wa UEFA wiki chache zilizopita huku akijivunia ufanisi katika kombe la Mabingwa na kimataifa.

Nahodha huyo wa Croatia aliisaidia timu yake hiyo kuwashangaza walimwengu, kwa kufika kwenye fainali ya Kombe la Dunia kule Urusi. Fauka ya hayo, Modric anajivunia ushindi wa kombe la mabingwa kwa mara ya tatu akiwa na Real Madrid msimu jana.


Kiungo huyo mtulivu ameendelea kumiminiwa pongezi katika mitandao ya kijamii huku makocha na wachezaji wenza wakitoa hisia zao. Kocha wa Croatia Zlatko Dalic amesema,” Modric ni nahodha wangu na anajituma sana. Ni kama msaidizi wangu pale uwanjani. Tuzo hili ni lake.” Naye Joachim Löw wa Ujerumani ambaye timu yake ilibanduliwa kwenye makundi, alimpongeza Modric kwa kudhihirishia ulimwengu kuwa kila jambo linawezekana, huku akisisitiza ubora wa nyota huyo hivi karibuni.


Inasubiriwa mno kujua ikiwa Modric atatawazwa mchezaji bora duniani katika tuzo za Ballon d’Or baadaye mwaka huu, atakapopambana na Cristiano Ronaldo na wengineo tena. Kiungo huyo amewashukuru wachezaji wenza wa Croatia na Real Madrid kwa kumsaidia kutwaa tuzo hilo,na kumtaja nahodha wa Croatia mwaka wa 1998 kama sanamu “idol” yake.


Mohamed Salah naye hakutoka mikono mitupu kwani alituzwa taji la PUSKAS kwa kufunga bao bora msimu jana, Liverpool dhidi ya Everton. Nyota huyo raia wa Misri hakung’aa kama ilivyotarajiwa kwenye Kombe la Dunia, baada ya kujeruhiwa kwenye fainali ya kombe la mabingwa, jambo lililomfanya kukosa mechi ya kwanza, Misri dhidi ya Uruguay.

Marta na tuzo lake


Mwanadada Mbrazili Marta alitwaa taji la mchezaji bora baada ya kuisaida timu yake kufuzu kwenye Copa America, walipobwagwa katika nusu fainali. Marta alifunga mabao kumi na matatu huku akisaidia ufungaji wa mengine sita. Binti huyo huichezea Orlando Pride.


Makocha pia walipata haki yao, Didier Deschamps wa Ufaransa akitajwa bora kwa kuiongoza “Les Bleus” kutwaa Kombe la Dunia kule Urusi. Reynald Pedros wa Lyon ndiye aliyetuzwa kocha bora wa kike.


Baada ya tuzo bora kumwendea Luka Modric, FIFA ilitangaza wachezaji kumi na moja waliong’aa mwaka huu.Thibaut Courtois wa Ubelgiji alibwagwa na David De Gea wa Manchester United na Uhispania, licha ya kutajwa kipa bora kwenye Kombe la Dunia. Nahodha wa Real Madrid Sergio Ramos aliwaongoza Marcelo, Dani Alves na Raphael Varane katika ulinzi.


Kiungo cha kati kilisheheni kiungo bora duniani Luka Modric pamoja na N’Golo Kante wa Chelsea huku Lionel Messi, Eden Hazard na Kylian Mbappe wakitawala kama viungo washambulizi. Katika nafasi ya kumaliza kazi ni mwuuaji na mshambulizi bora, Cristiano Ronaldo .

Leave a Comment