Chelsea, Arsenal, Juventus na Dortmund walabuliwa

Mbio za mibabe wengi wa soka bara Uropa ziliishia jangwani baada ya kulabuliwa, kurindimwa na kufedheheshwa mbele ya mashabiki wikendi iliyopita.

Crystal Palace iliifunza Chelsea jinsi ya kusakata soka ya kiume walipoalika Wanablues ugani Selhurst Park. Palace ambao walikuwa hawajashinda mechi yoyote tangu ligi kuu Uingereza kung’oa nanga, walipata mabao mawili ya kwanza ligini na ushindi muhimu kwa kocha Roy Hodgson aliyetwaa hatamu ya uongozi wa Palace majuzi.

Chelsea ilionekana kuchanganyikiwa kwenye robo ya kwanza ya mechi, pale Cesar Azpilicueta alipojifunga baada ya kushindwa kumkabili Yohan Cabaye. The Blues walirejea kwenye mechi dakika saba baadaye,Bakayoko akisawazisha baada ya kukamilisha krosi safi kutoka kwa Fabregas. Hata hivyo, Palace walionekana kulemea kikosi cha Antonio Conte kwa kumiliki mpira, pasi za kuaminika na maelewano si haba. Mambo hayo yalitia msumari wa mwisho kwenye kaburi la Chelsea, kwani Wilfried Zaha alifunga la pili dakika ya arobaini na tano huku akimwacha kipa wa Chelsea Thibaut Curtouis hoi.

Kwingineko ugani Vicarage Road, Watford waliilabua na kuicharaza Arsenal mabao mawili kwa moja Bellerin akijuta kwa kusababisha penalti iliyoizika timu yake.Per Mertesacker alikuwa wa kwanza kucheka na wavu, alipoifungia Arsenal dakika ya thelathini na tisa kwa kukamilisha kwa kichwa, kona iliyochongwa na Granit Xhaka.

Kipindi cha pili, kilianza kwa kasi huku Watford wakimiliki mpira na kuwanyima Arsenal nafasi ya kucheza mchezo wao wa gusa niguse. Maji yalizidi unga dakika ya sabini, pale Hector Bellerin alimwangusha Richarlison kwenye msambamba na kukabidhi Watford penalti iliyotiwa wavuni kwa ustaarabu na Troy Deeney. The Gunners walijipata waking’ang’ania alama moja kwenye mechi hiyo, huku jeraha la Laurent Koscielny likitia msumari moto kwenye kidonda cha Wanabunduki. Tom Cleverly aliifungia Watford bao la ushindi dakika ya tisini na kuwaadhibu mabeki wa Arsenal kwa kulaza damu na kutoelewana.

Kikosi cha RB Leipzig cha sherehekea ushindi dhidi ya Dortmund

 

Kule Italia kwenye Serie A, Juventus waliaibishwa nyumbani Turin kwa kupigwa, kulazwa na kubezwa mabao mawili kwa moja na timu ya Lazio.Douglas Costa, aliifungia Juventus bao la kwanza dakika ya ishirini na tatu, likiwa bao lake la kwanza tangu kujiunga na Old Lady kutoka Bayern Munich kwa mkopo.

Kipindi cha pili, kilishuhudia Lazio ikiilemea Juventus huku Ciro Immobile akisawazisha dakika ya arobaini na saba. Mabeki wa Old Lady walishindwa kujifunza kutoka kwa kosa la kwanza kwani kipa Gianluigi Buffon alimtega straika wa Lazio na kusawazisha penalti iliyofungwa kistadi na Immobile, dakika ya hamsini na nne. Juhudi za Juventus kujiokoa ziligonga mwamba kwani washambulizi wao  Gonzalo Higuain na Paulo Dybala walishindwa kutumia nafasi walizopata.

Ciro Immobile wa Lazio akisherekea bao lake la pili dhidi ya Juventus

Kule Ujerumani kwenye Bundesliga, rekodi ya Borussia Dortmund kutofungwa nyumbani ilifikia tamati  baada ya RB Leipzig, iliyopandishwa ngazi msimu jana, kutoka nyuma na kuichabanga timu hiyo mabao matatu kwa mawili.

Ushindi wa Dortmund ulidhihirika mapema baada ya Pierre-Emerick Aubeyang kucheka na wavu, dakika ya nne mbele ya mastaa wachanga wa Leipzig; Timo Werner, Emil Forsberg na Willi Orban. Hata hivyo, Marcel Sabitzer alisawazishia wageni hao dakika ya kumi huku Youssuf Poulsen mwenye asili ya Tanzania, akiipa Leipzig uongozi kwa bao la pili dakika ya ishirini na sita.

Dortmund walizidisha uvivu na makosa kwenye kipindi cha pili, Sokratis akipata kadi nyekundu na kuipa Leipzig penalti, iliyofungwa kwa weledi na Jean- Kevin Augustin dakika ya arobaini na tisa. Ugumu na mchecheto wa mechi hiyo,  uliongezeka dakika za sitini beki wa Leipzig Stefan Ilsanker alipofurushwa uwanjani kwa kadi nyekundu. Dortmund walituzwa penalti na Aubameyang kama ilivyo ada, akafunga la pili. Juhudi za Dortmund kupata la tatu ziligonga ukuta na Leipzig ikazoa alama zote tatu.

Wilfried Zaha asherehekea na wenzake wa Palace baada ya kuchapa Chelsea 2-1.

Yassina Terry.

Leave a Comment