Anayo majina sita,ndiye mshindi wa kombe LA bollan D’or wa mwaka 1995  na Mwafrika wa kwanza kufikia kiwango hicho,kutokana na usakataji,madoido na ubunifu wake katika soka,hayo ni kulingana na shirikisho LA soka duniani FIFA.si mwingine bali George Tawlon Mannoh Oppong Ousman Weah mwanasoka mstaafu aliyezaliwa nchini Liberia.

George Weah amejitosa katika ulingo wa siasa kama njia moja ya kuendeleza ushambulizi aliokuwa nao kwenye kabumbu.Miaka ya 1989, 1994 na 1995 ilishuhudia Weah akitajwa kuwa mchezaji bora wa karne hiyo huku akitambulika zaidi kwa kasi yake ugani na weledi wake wa kufunga mabao. FIFA ilimtaja gwiji huyo kama mwanzilishi wa washambulizi shupavu wa leo. Aidha, gwiji wa soka Mbrazili Pele alimtaja George Weah kwenye orodha ya wachezaji mia moja bora kuwahi kuonekana.

Weah alipotuzwa taji la mchezaji bora duniani, 1995

Taaluma yake kwenye Kabumbu

Baada ya kuanza taaluma yake nyumbani Liberia, George Weah alitumia miaka 14 kuzichezea timu za Ufaransa, Italia na Uingereza. Mkufunzi wa sasa wa Arsenal Arsene Wenger, ndiye aliyemleta Weah bara Uropa alipomsajili kule AS Monaco mwaka wa 1988. Miaka nne baadaye, Weah alijiunga na Paris Saint Germain ya Ufaransa na kutwaa taji la Ligue 1.Mwaka wa 1994, Weah alipata tuzo la mfungaji bora kwenye michuano ya Kombe la Mabingwa msimu wa 1994-1995.

Msimu uliofuata, Weah alihamia Italia na kujiunga na AC Milan alikotwaa taji la Serie A. Baada ya ufanisi huo, gwiji huyo aliguria Uingereza ambapo alichezea timu ya Chelsea kwa mkopo na ile ya Manchester City mwaka wa 2000. Baadaye mwaka wa 2003, Weah aliamua kutundika daluga na kukamilisha taaluma yake katika klabu ya Al Jazira.Weah aliwakilisha taifa lake kwenye mechi za Kombe la taifa Bingwa Afrika ( AFCON) kwa awamu mbili.

UBAGUZI WA RANGI

Weah alivunja pua la mchezaji wa FC Porto Jorge Costa mwaka wa 1996 baada timu yake ya AC Milan kutoka sare na Porto kwenye mechi za Kombe la Mabingwa. Weah alieleza kuwa alikuwa amechoshwa na kejeli pamoja na nyimbo za kumbagua kirangi kutoka kwa Jorge Costa kwenye michuano hiyo. Hata hivyo, Costa hakuadhibiwa kwa kosa hilo baada ya kesi hiyo kukosa ushahidi.

Suala hilo lilimfanya George Weah kufanyiwa upasuaji wa uso wake miezi kadha baadaye.

 

Siasa

Weah, alijitosa kwenye ulingo wa siasa mwaka wa 2005, alipowania urais na kupoteza kwa Ellen Johnson Sirleaf.  Hata hivyo, Mwaka wa 2011, Weah aliwania kiti cha naibu wa rais kwa tiketi ya Winston Tubman na kupoteza. Gwiji, huyo alijipata taabani kwani ilikuwa vigumu kwake kuteuliwa kwa kuwa hakuwa na kisomo cha hadhi ya juu. Miaka iliyofuata, Weah alitia bidii ya kujifunza Kiingereza na alifanya juhudi kuzungumza kwa ufasaha kama Barrack Obama. Baadaye mwaka wa 2014, Weah aliwania useneta na kushinda jambo lililompa motisha wa kuwania urais mwaka wa 2017.

Timothy Weah Mwanawe George Weah

Na kama ilivyo ada ya Waafrika hasa kitambo, kuwachagulia wanao kozi kwenye vyuo vikuu, Weah alifanya kinyume na kumruhusu mwanawe Timothy Weah kucheza kabumbu kuhakikisha kuwa wajihi na damu ya gwiji huyo inaendeleza sanaa ya soka ulimwenguni. Timothy alijiunga na Paris Saint Germain mwaka wa 2015, klabu ambayo babake mzazi aliichezea miaka ishirini iliyopita.

George Weah akiwania urais

Leave a Comment