PAUL PUT ATACHUKUA HATAMU ZA UKUFUNZI WA HARAMBEE STARS
Kwa kweli, hakuna zuri lisilokuwa na mwisho. Stanley Okumbi, alikuwa kocha wa Harambee Stars chini ya siku tano zilizopita,lakini kwa sasa hilo limo kwenye kurasa za kale. Hivi sasa ni rasmi kuwa Paul Put kutoka Ubelgiji amekwisha chukua hatamu za ukocha wa Harambee Stars, baada ya kutangazwa na Nick Mwendwa, rais wa shirikisho la soka FKF.
Okumbi, zamani Kariobangi Sharks alitundikwa mikoba ya ukufunzi wa timu ya taifa mwaka jana, katika mchakato wenye tashwishi. Kama nchi nyingi za Afrika zinazopendelea kocha Mzungu, Wakenya hawakumwamini Okumbi waliyesema hakuwa amekomaa kwa kazi hiyo.
Mtihani wa kwanza kwa Okumbi ulikuwa dhidi ya Mozambique mwezi Novemba mwaka huo(2016), mechi ambayo Stars walipata ushindi wa bao moja kwa nunge. Mwezi uo huo, Stars walipata ushindi sawia na huo dhidi ya Liberia nyumbani, na mashabiki wengi wakaanza kumuunga mkono Okumbi. Mechi hizo mbili zilikuwa za kirafiki.
Mwaka wa 2017 ulishuhudia Kenya ikicheza mechi saba za kirafiki, katika juhudi za kuimarisha kikosi. Mwezi Machi, Kenya iliambulia sare ya bao moja dhidi ya Uganda huku wakiichapa DR Congo mabao mawili kwa moja. Kwa mara nyingine sare ilijitokeza mwezi uliofuata, Kenya ilipochuana na Malawi.
Baada ya kucheza mechi tano bila kupoteza, kocha Okumbi alijipata taabani Juni mwaka huu baada ya Harambee Stars kulabuliwa na kurindimwa mabao mawili kwa moja na Sierra Leone, kule Free Town. Michael Olunga aliifungia Kenya bao la kufutia machozi dakika za mwisho mwisho, alipoinua mpira wa adhabu hadi wavuni. Mechi hiyo ilikuwa muhimu zaidi kwani ilikuwa ya kufuzu kwa Kombe la taifa bingwa Afrika ( AFCON).
Imani ya mashabiki ilianza kupungua nacho kikosi cha Stars kikazidi kudorora, huku wakiandikisha sare ya bao moja dhidi ya Mauritania na Mozambique, katika mechi za kirafiki zilizofuata
. Mwezi Oktoba, kidonda cha Okumbi kilizidi kutoneshwa na kutiwa msumari moto kwani Kenya ilicharazwa mabao mawili kwa moja na Iraq, kabla ya kuteswa bao moja kwa nunge na Thailand.
Sasa ni wazi kuwa Shirikisho la Soka nchini lilichoshwa na mtindo wa ukufunzi wa Okumbi, jambo lililolazimu kufurushwa kwake. Hata hivyo tetesi zipo kuwa Okumbi atapata kibarua cha hadhi ya chini kama naibu kocha au awe kwenye bodi ya usimamizi wa timu ya taifa.
Mbelgiji Paul Put, yumo nchini na alitangazwa kocha mpya katika kongamano la kila mwaka la FKF, kule Mombasa. Put aliwahi kuzifunza timu zaJordan na Burkina Faso ambayo ilimaliza nambari ya tatu kwenye kombe la taifa bingwa Afrika, mwaka wa 2013.
Mtihani wa kwanza kwa Put utakuwa mwezi Desemba tarehe tatu, Kenya dhidi ya Libya katika mechi za CECAFA ambapo Kenya ni mwenyeji. Wakenya wanatarajia kombe hilo wala si kufika fainali.
Hata hivyo, swali kuu ni:Je, Paul Put ataifikisha Harambee Stars katika kilele kinachotamaniwa na mashabiki?
Tukumbuke kuwa Put amewahi kufurushwa kwenye kabumbu kwa makosa ya kupanga matokeo ya mechi kabla ya mechi kuchezwa hasa!