Aliyekuwa kiungo mtengenezaji wa Arsenal na Borussia Dortmund, Tomas Rosicky amestaafu. Gwiji huyo aliyependwa sana kwa mchezo wake wa gusa niguse alitangaza kustaafu hiyo jana, katika maongezi na vyombo vya habari kule Jamhuri ya Czech.
Rosicky alisema kuwa ameafikia uamuzi huo kwa kuwa umri wake wa miaka 37 haumruhusu kuendelea kucheza kabumbu ya kulipwa. Nyota huyo alikuwa amerejea Sparta Prague baada ya kuondoka Emirates, na kandarasi yake ilikuwa ikamilike mwaka ujao Juni.
“Baada ya kufikiria na kuzingatia masuala kadhaa, nimeamua kustaafu kwa kuwa sipo katika hali shwari kuendelea kucheza.” Alisema Rosicky. ” Nashukuru Sparta Prague kwa kunilea na kuwa waanzilishi wa ufanisi wangu. Nawashukuru kwa kunikubalia kusema kwaheri kwa mashabiki na mahali hapa ambapo napenda zaidi.”
Rosicky alianza kuchezea nchi yake ya Czech mwaka wa 2000 na kufanywa nahodha wa timu ya taifa mwaka wa 2006. Kiungo huyo alistaafu kutoka kwa kandanda ya kimataifa mwaka wa 2016 baada ya kushiriki mechi mia moja na tano na kufunga mabao ishirini na tatu.
Rosicky aliisaidia Sparta Prague kushinda mataji matatu ya ligi kuu ya Czech, tangu mwaka wa 1998 kabla ya kujiunga na Borussia Dortmund mwaka wa elfu mbili (2000). Gwiji huyo aliwagharimu Dortmund paundi kumi na nane (£18M) na kuwa mchezaji ghali zaidi Ujerumani enzi hizo.
Kule Bundesliga, Rosicky aliichezea Dortmund kwa miaka sita huku akishinda ligi kuu msimu wa 2001-2002, pamoja na kuwa timu ya pili kwenye kombe la UEFA na lile la DFB LigaPokal mwaka wa 2003.
Baada ya ufanisi huo, Rosicky alijiunga na Arsenal ya Uingereza mwaka wa 2006 na kushinda mataji mawili ya FA msimu wa 2014-2014 na 2014-2015. Aidha , Arsenal ilishinda taji la ngao ya jamii (Community Shield) mwaka wa 2014.
Taaluma ya Rosicky kule Arsenal ilikumbwa na majeraha kadhaa lakini hilo halikupunguza umaarufu wake kwenye mashabiki. Mbinu zake katikati mwa uwanja na mabao yake ya kupigiwa mfano yalimfanya kipenzi cha wengi.
Rosicky alirejea kwenye klabu yake ya utotoni Sparta Prague mwaka wa 2016 baada ya kandarasi yake kukamilika na Arsenal.
Gwiji huyo anajivunia mataji kadhaa ikiwemo tuzo la mchezaji bora wa Czech mwaka wa 2001, 2002 na 2006. Rosicky pia alishinda tuzo la mfungaji bora mwaka wa 2006 akiwa na timu ya taifa, na tuzo la chipukizi wa mwaka 1999.
Mesut Ozil alisema, ” Hongera kwa mchezaji mwenye roho nzuri aliyekuwa na ufanisi si haba kwenye taaluma yake. Nakutakia kila la heri unapostaafu.”
Naye Theo Walcott akaongeza, ” Nakutakia kustaafu kwema . Najivunia kuwahi cheza nawe na naenzi wakati tuliokuwa pamoja kiwanjani na nje ya uwanja.”