ZANZIBAR INAONGOZA KUNDI A

Ovella Ochieng(jezi 7) wa Kenya dhidi ya mabeki wa Zanzibar, Jumamosi.

 

Kikosi cha Kenya, Harambee Stars kimejipata taabani kwa mara nyingine baada ya kuambulia sare tasa dhidi ya Zanzibar, siku ya Jumamosi. Chini ya ukufunzi wa kocha mpya Paul Put, Stars imeshinda mechi moja tu huku wakiandikisha sare kwenye mechi mbili.

Mabao ya Duncan Otieno na Masoud Juma dhidi ya Rwanda, yalikuwa yameanza kuziponya roho za mashabiki lakini sare dhidi ya Libya haikupendeza. Stars sasa watalazimika kuilaza Tanzania siku ya Jumatatu ili kufufua ndoto ya kufuzu kwenye nusu fainali.

Zanzibar inaongoza kundi A kwa alama saba huku Kenya ikifuata kwa alama tano. Libya ni ya nne kwa pointi tatu huku Tanzania ikishikilia mkia. Hii inamaanisha kuwa Libya ikiilaza Zanzibar Jumatatu nayo Kenya ichapwe na Tanzania, basi Libya itafuzu. Libya imeandikisha sare kwenye mechi tatu ilizocheza.

Kassim Khamis wa Zanzibar akisherehekea bao lake dhidi ya Tanzania.

Zanzibar wameshinda mechi mbili mfululizo , wakiilaza Rwanda mabao matatu kwa moja kabla ya kutoka nyuma siku ya Alhamisi na kuirindima Tanzania, mawili kwa moja. Ibrahim Ahmada na Kassim Khamis wamekuwa nguzo muhimu kwenye kikosi cha Zanzibar Heroes kwani wamecheka na wavu katika mechi muhimu.

Tanzania wamekwisha yaaga mashindano kwani wana alama moja pekee kwenye mechi tatu. Kilimanjaro Stars watacheza mechi yao ya mwisho Jumatatu dhidi ya Kenya, kabla ya kuaga mashindano rasmi. Timu hiyo imeandikisha bao moja pekee, bao lililofungwa na Himid Mao Alhamisi, Kilimanjaro Stars walipocharazwa na Zanzibar.

 

Katika kundi lilo hilo, vijana wa Kagame yaani Rwanda wameyaaga mashindano baada ya kuandikisha ushindi mmoja tu kwenye mechi nne walizocheza. Kigali Stars walicharazwa mabao mawili kwa nunge na Kenya kabla ya kurindimwa mabao matatu kwa moja na Zanzibar.

Mechi iliyofuata waliambulia sare tasa dhidi ya Libya ila pointi hiyo moja haikuwaokoa. Rwanda ilifanikiwa kupata pointi tatu dhidi ya Tanzania siku ya Jumamosi Ila walikuwa wamekisha chelewa.

Innocent Nshuti aliifungia Rwanda bao la ufunguzi kipindi cha kwanza kabla ya Daniel Lyanga kusawazishia Kilimanjaro Stars dakika ya ishirini na tisa.Mambo yalizidi kunyooka kwa Rwanda kwani Birahimire Abeddy aliongeza la pili dakika ya sitini na sita.

Ushindi huo uliiweka Rwanda kwenye nafasi ya tatu kwa pointi nne alama moja nyuma ya Kenya na tatu nyuma ya Zanzibar. Timu za Libya na Tanzania zinashikilia nafasi za nne na tano mtawalia.

Leave a Comment