Klabu ya Sharks inayoshiriki ligi ya Chuo Kikuu cha Moi, iliibetua, ikaiburura na kuilaza timu kuu ya chuo hicho, Field Marshalls mabao matatu kwa mawili, ugani Upperhill.
Mechi hiyo ambayo kwa kawaida huzua mhemko mahasidi hao wanapogaragazana, ilishuhudia ubabe wa aina yake huku refarii Euro akipongezwa kwa maamuzi ya hekima.
Sharks walikuwa wa kwanza kucheka na wavu walipotunukiwa mkwaju wa penalti, baada ya mlinzi wa Marshalls kumtega José kwenye kijisanduku. Majukumu ya upigaji yalitwikwa Mogire ambaye hakusita kutia mpira kimiani, kwani kipa Charles alienda magharibi huku mpira ukiwekwa Mashariki.
Marshalls walitia fora kukomboa bao hilo, lakini shuti la Ishmael almaarufu Ishy lilipanguliwa na kipa wa Sharks, Alfred Ndemo. Mchecheto ulikuwa si haba kwani Chris alishirikiana vyema kabisa na Job almaarufu Pirlo kwenye kushambulia ingawa mikiki yao ilipanguliwa, kuokolewa na wakati mwingine kupaa juu ya mtambaa panya.
Katika harakati za kutafuta bao la kusawazisha, Marshalls walipoteza umiliki wa mpira na Sharks wakapata bao la pili kwa shambulizi la kushtukiza. Kipa Alfred alipiga shuti la mbali lililotua miguuni mwa Johnny naye akamwandalia mshambulizi wao hatari, Mogire. Juhudi za Charles Brian kuokoa timu yake ziligonga mwamba, kwani alipojaribu kuondoa mpira huo, Mogire alitumia kichwa chake na kupiga mpira huo mbele, kisha akatumia mbio yake kumwacha kipa na kujaza mpira ndani ya wavu.
Wasiwasi ulizidi kumwingia kocha wa Marshalls Alphonce huku akimpumzisha Kenas na kuweka Eric kwenye ubavu wa kushoto. Ghadhabu ya kocha iliwalazimu Marshalls kurejea mechini, kwa kupiga pasi za uhakika na kumiliki mchezo kwenye robo ya pili ya mechi.
Kwa kweli, atafutaye hachoki kwani Marshalls walifanikiwa kupata bao la kusawazisha dakika ya thelathini na tatu kupitia kwa Pirlo aliyeujaza mpira wavuni baada ya kiki la Pius kupanguliwa hapo mwanzo.
Bao hilo liliwatia ukakamavu wanaMarshalls ila walishindwa kuhimili mashambulizi ya kushtukiza yaliyoandaliwa na Sharks.Watoto wa nyumbani waliadhibiwa kwa mara ya tatu kwa shambulizi la kushtukiza, baada ya Johnny kupokea mpira kutoka Edwin Maru na kisha kumwandalia Vincent aliyewachenga walinzi na kipa wa Marshalls, na kufunga bao la tatu.
Kipindi cha kwanza kilikamilika Sharks wakiongoza mabao matatu kwa moja huku refa Euro akiashiria muda wa mapumziko.
Nusu ya pili ya kipute hicho, ilishuhudia kocha Alphonce akileta kikosi kipya ugani huku meneja Anderson Imbova wa Sharks akishikilia kikosi alichoanza nacho. Marshalls walimleta Kelvin kuchukua nafasi ya mlindalamgo Charles Brian, huku Victor, Chege na Mohammed wakishikilia ulinzi. Kikosi kipya cha Marshalls kilionyesha ukakamavu na kujiamini huku Otto akileta krosi nzuri zilizozua hatari .
Hata hivyo, Sharks ilijikaza kisabuni kuhimili mashambulizi na kutumia mikiki ya adhabu waliyopewa. Dakika ya hamsini na tano, Edwin alichezewa vibaya tena na kuumia huku Alex akichukua nafasi yake. Refarii aliwatunuku Sharks mkwaju wa fauli, ila kiki stadi la Mogire lilipita juu ya mtambaa panya japo kiduchu tu.
Dakika tano baadaye, Otto alionekana kuwalemea walinzi wa Sharks alipoingia vizuri kwenye msambamba na kumwandalia Muia pasi maridadi, na mpira kujaa wavuni.
Taswira ya mechi ilianza kubadilika huku Sharks wakionekana kuingiwa na wasiwasi. Katika takwimu zao za kushikilia ushindi huo kipa Alfred alianza kupoteza muda kosa ambalo nusura lizalishe bao la tatu. Refa aliizawidi Marshalls na kiki la bwerere ndani ya kijisanduku, lakini Don alipaisha kiki lake hivyo kupoteza nafasi hiyo finyu.
Mechi hiyo ilikamilika Marshalls wakijutia kupoteza nafasi zao huku Sharks wakisherehekea ustadi wao wa kuandaa mashambulizi murua ya kushtukiza.
Marshalls sasa watachuana na Wakongwe wa kikosi hicho Jumamosi hii na watajizatiti kurejesha hadhi yao.