SIASA YAANGAMIZA MICHEZO; KENYA

JUBILEE, NASA! Naam huu ndio msemo wa siku hapa Kenya. Utakuta mashabiki wa mirengo hiyo wakibishana mitandaoni, kila mmoja akijaribu kuonyesha jinsi mrengo wake in bora. Si wazomei hao, ila inasikitisha kuona hali ya michezo  nchini ikizidi kudorora, siku baada ya nyingine.

Juni mwaka huu, Kenya ilinyang’anywa fursa adimu ya kuandaa michuano ya CHAN inayohusisha timu za bara zima la Afrika. Wengi watasema kuwa viwanja vyetu havikuwa katika hali ya kimataifa lakini, ni taifa lipi litatuma timu yake ije kucheza katika nchi ambayo vitoa machozi na maandamano ndio ada?

Kuandaa CHAN kungeibua nafasi nzuri mno ya kupevua machipukizi wetu na ingesaidia kuinua hadhi ya Kenya, katika ulimwengu wa spoti. Si vyema kuzidi kuongelea suala hilo kwani nitakuwa natonesha kidonda cha mwanaspoti yeyote kama mimi. Muhimu ni kuwa, taifa la Morocco litaandaa CHAN mwakani na Wakenya watalazimika kutizama mechi hizo runingani.

 

Wikendi iliyopita, ligi kuu nchini ; Sportpesa Premier League ilikosa kuendelea kwa sababu za kiusalama. Ligi za daraja za chini pamoja na michuano ya CHAPA NDIMBA inayohusu vijana wa chini ya miaka ishirini, ilikwama. Utakubaliana nami kuwa talanta inalipa mno katika dunia ya sasa na vijana wanaocheza kwa sasa wanapigania ndoto zao.

Mwezi Agosti, katika awamu ya kwanza ya uchaguzi mechi ziliahirishwa . Hivi sasa, ligi kuu nchini imesalia na mechi tano kabla ya kutamatika na hali tete ikizidi, ligi italemaa. Timu ya taifa, Harambee Stars ina mechi ngumu dhidi ya Ghana mwakani katika juhudi za kufuzu kwenye kombe la taifa bora Afrika,AFCON. Hii inamaanisha kuwa, sharti ligi ikamilike mapema ili wachezaji watakaoitwa kambini, waanze mazoezi.

Siasa zimeingilia vilabu ambapo kusajiliwa kwa wachezaji kunazingatia ukabila. Wakati mwengine sharti mchezaji atoe hongo ili afanye majaribio. Ikiwa huna ” connections” basi ndoto yako ya kucheza kabumbu hufa.

Mapema mwaka huu, kampuni ya uwekezaji; Sportpesa ilitishia kujiondoa nchini baada ya kukorofishana na washikadau serikalini. Tukumbuke kuwa kampuni ya Supersport ilijiondoa na athari zake tuliziona. Supersport ilikuwa inafadhili vifaa vya mazoezi, jezi za timu na marupurupu ya wachezaji. Walipoondoka, timu kadhaa zilitatizika huku Muhoroni na Sony Sugar zikikosa kulipa wachezaji kwa miezi kadhaa.

Shukran kwa Sportpesa kwa kuokoa jahazi. Kampuni hiyo ilifadhili ligi kuu nchini, ikafadhili Gor Mahia na AFC Leopards na matunda yake ni wazi. AFC ilitwaa taji la GO TV Shield wiki mbili zilizopita nayo Gor imetawazwa ubingwa wa Ligi kuu nchini. Timu hizo mbili zitawakilisha Kenya katika michuano ya vilabu Afrika almaarufu Continental Cup.

Tunahitaji wafadhili zaidi ili kuinua michezo nchini. Ili kuwavutia wawekezaji sharti taifa liwe tulivu kwa minajili ya mandhari safi ya biashara. Inahuzunisha kuona vijana nchini wakiacha kucheza kabumbu katika umri wa miaka ishirini wakati Charly Musonda na Rashford wanavuna mamilioni katika umri huo huo.

    Humphrey Mieno amwacha mlinzi wa Tusker hoi zamani hiyo akiwa Sofapaka

Leave a Comment