Jumapili, Oktoba mosi ilishuhudia ufunguzi wa nusu fainali ambapo bao Ali Hussein liliipeleka Egerton Njoro kwenye fainali baada ya mechi ngumu kupindukia dhidi ya Laikipia. Semi fainali ya pili iliambulia sare ya bao moja kati ya UoE na Maasai Mara baada ya Betto Hassan kusawazishia Maasai Mara kipindi cha pili kwa njia ya penalti. Hata hivyo Wamaasai hao walijikwamua kwa njia ya matuta na kuilaza UoE matatu kwa mawili na kufuzu kwenye fainali.

 

Timu ya Egerton kina dada iliilaza Laikipia matatu kwa moja, Victory Oudu, Jackline Musangi na Stephanie Mugatsia wakifunga. UoE nao wakainyeshea Moi Main Campus matatu kwa nunge na kufuzu kwenye fainali.

 

Katika kutafuta tatu bora, timu ya Moi Main Campus ilijikwamua kwa kuilabua Laikipia mawili kwa nunge huku UoE ikiilaza Laikipia matatu kwa mawili kwenye penalti kwa wanaume.

 

Fainali ya kina dada kati ya Egerton na UoE ilidhihirisha wazi uwezo wa kina dada huku timu zote zikicheza mchezo wa kuridhisha. Hata hivyo, UoE iliwazidi Egerton nguvu kwa kuilaza mabao mawili kwa nunge Shamilla Bengo na Marylyn Wambua wakicheka na wavu.

 

Egerton Njoro na Maasai Mara walikutana kwa mara ya pili wakati huu ikiwa kwenye fainali huku ikikumbukwa KUSA wawili hao walikuwa kwenye kundi moja. Katika mechi za makundi Egerton iliilaza Maasai Mara mawili kwa nunge Kung’u na Ali Hussein wakifunga.Fainali hii ilikuwa ngumu huku mashabiki wakibaki kumeza mate kwa Soka safi iliyochezwa. Egerton kwa mara ya pili iliilemea Maasai Mara kwa kuilaza bao moja komo ufe baada ya Ali Hussein kukamilisha kona kwa kichwa safi kilichomwacha kipa wa Maasai Mara hoi.

Yassina Terry.

Leave a Comment