Kikosi cha Wazito chasherehekea baada ya kutwaa Jamhuri Cup.

 

 

Klabu ya Wazito iliyopandishwa daraja majuzi iliishangaza Rangers  siku ya Jumanne, baada ya kuirindima bao moja kwa nunge. Mechi hiyo ilisakatwa katika uga wa Moi Sports Centre; Kasarani katika sherehe za Jamhuri.

Aliyekuwa mshambulizi wa Tusker John Mabia alifunga bao hilo muhimu baada ya kuingizwa kama nguvu mpya. Mabia alikamilisha krosi safi iliyochongwa na Mark Odhiambo huku kipa wa Rangers Farouk Sikhalo akiachwa hoi.

 

“Ushindi huu ni dhihirisho wazi kuwa timu yangu iko imara. Kwa sasa tunaelekea kwenye matayarisho ya msimu mpya na ushindi huu umenipa moyo. Nina kikosi ambacho kinafikiria kushinda kila mechi,” alisema kocha wa Wazito Frank Ouna.

 

Kocha wa Rangers Sammy Omollo “Pamzo” alimtumia Farouk Sikhalo kama mlindalango, ili kujaza nafasi ya Patrick Matasi ambaye ana majukumu kwenye kikosi cha Harambee Stars. Dennis Mukaisi aliongoza safu ya ushambulizi.

Wazito FC ilipandishwa ngazi baada ya kuongoza ligi pana.

 

Kikosi cha Wazito kilijumuisha Moses Otieno na Harun Nyakha, waliojiunga na mabingwa hao kutoka Posta Rangers na AFC Leopards mtawalia.

Wazito walishambulia mno huku mkwaju wa Joseph Waithira ukiokolewa na Sikhalo. Kwa upande wao, Rangers walilinda lango na kushambulia si haba kwani Joseph Nyagah karibu acheke na wavu. Hata hivyo fataki ya Nyagah haikufua dafu kwani mpira ulipaa juu mtambaa panya.

 

John Mabia aliingia dakika ya sitini na tisa kuchukua nafasi ya Joseph Waithira, kabla ya kufunga bao maridadi dakika ya themanini na nane. Rangers walifanya juhudi zote kusawazisha huku Titus Achesa akiinua krosi hatari lakini Wazito walinusurika.

 

Akizungumza baada ya mechi, kocha wa Rangers alikiri kusikitishwa na matokeo hayo. ” Tulitengeneza nafasi nyingi ambazo hatukutumia. Sasa tumepoteza mechi dakika za mwisho kwa kukosa kumakinika.” Alisema Sammy Omollo “Pamzo”.

 

 

Leave a Comment