Aliyekuwa kiungo mshambulizi wa AC Milan na Real Madrid, Ricardo Izecsano dos Santos Leite almaarufu Kaka, ametundika dalugha. Kaka aliandika ujumbe wa kustaafu kwake kwenye ukurasa wake wa Instagram, mapema leo. Nyota huyo amestaafu akiwa na umri wa miaka thelathini na tano, huku akijivunia rekodi nzuri ya mataji na ufanisi si haba kama mchezaji.
Kaka alianza taaluma yake ya kabumbu akiwa na umri wa miaka kumi na minane, katika klabu ya Sao Paulo, nyumbani Brazili. Baada ya kuchezea klabu hiyo kwa miaka miaka mitano Kaka alijiunga na AC Milan ya Italia, mwaka wa elfu mbili na tatu (2003).
Ni katika klabu hiyo ya Italia ambapo Kaka alijipatia umaarufu tele baada ya kuishindia timu hiyo Kombe la Klabu Bingwa bara Uropa mwaka wa elfu mbili na saba.
Milan walitajwa mabingwa wa bara hilo kwa mara ya saba , huku Kaka akijivunia kufunga mabao kumi kwenye michuano hiyo.
Ushindi huo ulimsaidia Kaka kushinda tuzo la mchezaji bora duniani almaarufu Ballon D’Or mwaka huo (2007). Kaka alijitambulisha kama kiungo mshambulizi maridadi wa nyakati zake huku akiwa mchezaji wa mwisho kutwaa taji la Ballon D’Or kabla ya Messi na Ronaldo.
Miaka miwili baadaye Kaka aligura AC Milan na kujiunga na Real Madrid kwa rekodi ya dunia enzi hizo ya kima cha paundi sitini na nane (€68M). Hata hivyo, mambo hayakumwendea sambamba kule Madrid kwani hakuweza kudhihirisha ubabe wake kama kule Milan.
Licha ya hayo, Kaka alishinda taji la Copa del Rey na Real Madrid mwaka wa 2011 huku akishinda taji la ligi kuu almaarufu Laliga mwaka mmoja baadaye.
Kaka alirejea AC Milan mwaka wa 2013 kwa uhamisho wa bwerere baada ya kukamilisha kandarasi yake na Real Madrid. Gwiji huyo alichezea klabu hiyo kwa msimu moja, kabla ya kuhamia Marekani.
Kaka alizinduliwa kama uso wa ligi ya Marekani; Major League Soccer kule Orlando City mwaka wa 2014. Hata hivyo, Orlando City ilimpeleka Kaka kule Sao Paulo kwa mkopo, huku nyota huyo akipata fursa nyingine ya kuchezea klabu yake ya utotoni.
Mwaka wa 2015, Kaka alifunga bao la kwanza kwa Orlando City na kuwa mchezaji aliyelipwa hela nyingi kwenye ligi hiyo, kwa miaka mitatu, kabla ya kuhama mwezi Oktoba mwaka wa 2017.
Mwezi Novemba , taarifa zilienea kwamba Kaka alikuwa anapanga kujiunga na Guizhou Hengfeng Zhicheng inayoshiriki ligi kuu kule Uchina.
Kaka atakumbukwa sana kwa mchango wake kwa timu ya taifa ya Brazili ,hasa baada ya kushinda Kombe la Dunia la mwaka wa 2002, lililoandaliwa kule Japan. Bingwa huyo ameifungia Samba Boys mabao ishirini na tisa kwa mechi tisini na mbili . Hata hivyo, Kaka hakushiriki kombe la dunia mwaka wa 2014 licha ya kuwa liliandaliwa huko Brazili.
Kwa mara nyingine, Kaka alikosa michuano ya Copa America Centenario wakati huku kwa sababu ya jeraha.
Ligi kuu ya Uhispania; Laliga imemsifia Kaka kwenye ukurasa wao wa Twitter huku wakimtakia kila la heri.
Gwiji huyo amesema kuwa anaangazia kuwa kocha au mkurugenzi wa kabumbu katika baadhi ya vilabu alivyochezea, huku AC Milan ikiwa tayari kukabidhi majukumu hayo. Aidha, Kaka amewasihi mashabiki waendelee kumuunga mkono atakapoanza ukufunzi.
” Kwamba nilikuwa mchezaji bora haimaanishi nitakuwa kocha bora, ila nitafanya niwezalo kufanikiwa katika taaluma hiyo mpya,” alisema Kaka.