Harambee Stars yasherehekea baada ya kukabidhiwa kombe la CECAFA

 

 

Timu ya taifa Harambee Stars ndio mabingwa wa kombe la CECAFA mwaka huu baada ya kuicharaza na kuilabua Zanzibar, mabao matatu kwa mawili kwenye fainali. Mechi hiyo iliyogaragazwa kule Machakos, ilizua mchecheto na mhemko si haba, hadi dakika ya mwisho.

 

Kenya ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Ovella Ochieng dakika ya tano, kwa njia ya mpira wa adhabu baada ya Whyvonne Isuza kuchezewa vibaya na Abdulazziz Makame.

 

Ochieng aliiuchonga mkiki huo kwa njia stadi ajabu kwani hakuna mtu aliyeugusa hadi wavuni. Kipa wa Zanzibar alibaki akiruka kuondoa lawama kwani hakuweza kuliokoa jahazi.

 

Kipindi cha kwanza kilikamilika kwa bao hilo moja huku Harambee Stars ikimiliki mchezo. Hata hivyo, Zanzibar iliingia ugani na msisimko mpya kipindi cha pili huku fataki za Ibrahim Ahmada na wengineo zikiokolewa na Patrick Matasi.

 

Kama walivyonadi wahenga mgaagaa na upwa hali wali kavu, Zanzibar ilisawazisha dakika za lala salama na kubadilisha taswira ya mechi. Bao hilo lililochongwa na Khamis Musa kunako dakika ya themanini na saba, lilikuwa adhabu kubwa kwa walinzi wa Stars.

 

Ovella Ochieng asherehekea bao lake na wenzake wa Harambee Stars

Dakika tisini zilikamilika kwa sare ya bao moja na kulazimu kuchezwa kwa muda wa nyongeza. Robo hiyo ilishuhudia mabao ya kushtukiza kwani Masud Juma alifungia Kenya la pili dakika ya tisini na saba, baada ya Harambee Stars kutengeneza shambulizi murua la kushtukiza.

 

Furaha ya Wakenya ilidumu kwa dakika chache kwani Khamis Musa alifunga tena, wakati huu akichukua mpira kutoka kwa mlinzi wa Kenya Musa Mohammed. Nahodha huyo wa Kenya, alifanya kosa katika kuondoa mpira na Khamis hakusita kutia mpira wavuni.

 

Robo ya kwanza ilikamilika kwa mabao hayo mawili kwa pande zote, huku timu zote zikizuia vyema kwenye robo ya pili. Matokeo hayo yalilazimu kupigwa kwa matuta almaarufu penalti.

 

Penalti mbili za kwanza kwa Zanzibar ziliondolewa na Patrick Matasi, huku Jockins Atudo akifungia Kenya penalti ya kwanza.  Hata hivyo, mkwaju wa Duncan Otieno uliokolewa na kipa wa Zanzibar lakini Matasi aliokoa mkwaju wa tatu wa Zanzibar Heroes.

 

Wesley Onguso Arasa na Patilla Omotto waliifungia Kenya penalti nyingine na kuhakikisha wanatwaa taji hilo. Mlindalango Patrick Matasi ndiye aliyetawazwa tuzo la mchezaji bora wa mechi hiyo huku akiandikisha historia kwa kuokoa penalti tatu.

Leave a Comment