The Minnows ya Zanzibar imejikatia tikiti ya fainali hii leo, baada ya kuicharaza Uganda Cranes mabao mawili kwa moja. Mechi hiyo iligaragazwa katika uga wa Moi kule Kisumu.
Abdulazziz Makame alikuwa wa kwanza kucheka na wavu kwa upande wa Zanzibar kunako dakika ya ishirini na mbili, kabla ya Derrick Nsibambi kusawazishia Cranes dakika sita baadaye.
Uganda walijitahidi kwa udi na uvumba kupata uongozi wa mechi hiyo, lakini mikiki ya Milton Karissa na Mutyaba ilipanguliwa na wakati mwengine kutolenga shabaha.
Mipango ya Uganda ilizidi kusambaratika dakika ya hamsini na tano, baada ya Nsubunga Joseph kupata kadi nyekundu. Mwiba huo uliwapa nguvu Minnows kwani Mohammed Issa aliongeza la pili dakika ya hamsini na saba, bao lililoipa Zanzibar ushindi.
The Minnows watachuana na Harambee Stars kwenye fainali Jumapili hii, kule Machakos kwenye uga wa Kenyatta. Kenya walifuzu siku ya Alhamisi kwenye nusu fainali ya kwanza, walipoilaza Burundi bao moja kwa nunge.
Whyvonne Isuza alifunga bao hilo muhimu katika muda wa mazidadi, baada ya kupata krosi safi kutoka kwa Dennis Sikhayi. Mechi hiyo ilikamilika kwa sare tasa kwenye muda wa kawaida na kulazimu dakika thelathini za nyongeza.
Uganda sasa watapigania nafasi ya tatu Jumapili hiyo hiyo, watakopochuana na Burundi saa saba unusu mchana. Fainali itang’oa nanga saa kumi kamili saa za Afrika Mashariki.