Nahodha wa Gor Mahia Harun Shakava ainua taji la Supercup baada ya kuilaza AFC Leopards

 

Gor iliilaza Ingwe bao moja kwa nunge na kutwaa taji hilo

 

Kocha wa Gor Mahia Dylan Kerr amemmiminia sifa nahodha wa kikosi chake Harun Shakava, kwa kuonyesha mchezo mwema siku ya Jumapili alipoifungua K’Ogalo bao la ushindi.

 

Itakumbukwa kuwa Shakava aliteuliwa kama nahodha baada ya Musa Mohammed aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo, kujiunga na FK Tirana ya Albania, mapema mwaka huu.

Mechi hiyo ya taji la Supercup ilikuwa ya kwanza kwa Shakava kama nahodha, na ilimchukua dakika arobaini na tatu tu kuwaadhibu AFC Leopards.

Duncan Otieno wa AFC ( Kushoto) akimkaba Meddie Kagere wa Gor Mahia (Kulia)

 

Licha ya ushindi huo, Kocha Kerr alitoa lawama kadha kuhusu maamuzi ya refarii huku akisema kuwa refa Peter Waweru alikosa kuwatunuku Gor Mahia penalti mbili za wazi. Nusura mashabiki wa K’Ogalo wazue rabsha kwenye mechi hiyo baada ya refarii kupepesea chini lawama hizo.

 

Kwa upande wake, kocha wa AFC Leopards Robert Matano alisema kuwa hakuona tukio lolote lililostahili penalti.

Kikosi cha AFC kilionekana kunyong’onyea huku wakishindwa kushirikiana ipasavyo. Haha hivyo kocha Matano aliwapongeza vijana wake huku akiwasihi kujikakamua kwenye mechi zijazo.

Kipa wa Gor, Boniface Oluoch asherehekea bao lao dhidi ya Ingwe

 

Aidha, Matano aligusia suala linalosambaa kuwa eti wachezaji wa Ingwe walikataa kushiriki mazoezi pamoja na kukwepa mechi kwa madai ya kutolipwa. Kocha hiyo alionekana kukerwa na tabia hiyo, na kuwaomba wachezaji wa AFC Leopards wazingatie mchezo kwani si jukumu lao kujua malipo yatokako, kwa kuwa kuna ofisi inayoshughulikia mishahara ya wachezaji.

 

Matano ambaye ameshtumiwa kwa kuweka sure ngeni kikosini, alitumia wachezaji wanne tu wa kikosi cha kwanza; kipa Gabriel Andika, walinzi Dennis Shikayi, Salim Abdalla na kiungo Duncan Otieno.

 

Ligi kuu nchini itang’oa nanga wikendi ijayo, huku Gor ikiikaribisha Nakumatt FC Jumapili, nao AFC Leopards wachuane na Posta Rangers.

 

 

Leave a Comment